MWAJUMA JUMA NA TUWERA JUMA, MCC
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wameishauri serikali kufuatilia pale inapotoa agizo la kupunguzwa ama kufutwa kodi ili kubaini utekelezwaji wake ambao una lenga la kuwapa unafuu wa maisha wananchi.
Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Ali Suleiman Ameir wakati akiwasilisha mapendekezo ya mpango wa maendeleo na bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022, katika kikao cha baraza la Wawakilishi kinachoendelea.
Alisema serikali hufanya uamuzi mzuri wa kuwajali wananchi wake kwa kuwapunguzia kodi ama kuifuta, lakini ni vyema uwepo ufuatiliaji ili kuhakikisha kwa kiasi gani wananchi wake wanafaidika na punguzo la kodi.
Hata hivyo alisema katika marekebisho ya sheria ya usimamizi wa fedha za umma namba 12 ya mwaka 2016 ambayo yamefuta tozo na ada mbali mbali za serikali za mitaa, lakini kamati imebaini kutokushirikishwa ipasavyo serikali hizo na kusababisha taasisi kutofikia malengo ya ukusanyaji wa mapato.
Alifahamisha kamba kutokana na hali hiyo kumesababisha kutomudu gharama za uendeshaji wa mamlaka hizo kwa kufanya usafi wa miji na kushindwa kuanzisha miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
Mwenyekiti huyo aliishauri Serikali wakati wa kuandaa bajeti kufanya uchunguzi wa kina wa makisio ya mapato na uwezo wa vyanzo vya mapato kwa kuzingatia hali ya mwelekeo wa uchumi kulingana na mazingira ya ndani na nje ya nchi.
Aidha alisema katika mwaka wa fedha 2020/2021 kamati imebaini kwamba asilimia kubwa ya matumizi ya serikali yametumika katika kazi za kawaida kuliko kazi za maendeleo.
Alisema hali hiyo ndio ambayo husababisha utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo kusuasua kutokana na ukosefu wa fedha ambazo kwa kiasi kikubwa ni mikopo na ruzuku kutoka kwa washirika wa maendeleo.
Akichangia bajeti hiyo, Mwakilishi wa jimbo la Mfenesini, Machano Othman Said alisema sekta binafsi ni muhimu hivyo inahitaji kusimamiwa vizuri ili isaidie serikali katika uchumi wa nchi.
Alifahamisha kwamba kuna watu wanadhani kwamba wale ambao hufanya kazi katika sekta binafsi wamekosa kazi lakini watu hao wengi wao wameacha kazi serikalini na kujiunga sekta binafsi, na wamekuwa mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.
Naye Mwakilishi wa jimbo la Micheweni, Shamata Shaame Khamis, alisema katika kuimarisha sekta ya uchumi wa buluu ni vyema jitihada zikachukuliwa kuwaelimisha wananchi juu ya dhana hiyo na faida yake kwao.
“Ukweli ni kwamba bahari tunayo na wavuvi wapo lakini kwa vile ambavyo tunaitumia bahari zao ni dhahiri hatuwezi kuitumia vizuri kama hawatopatiwa nyenzo na ujuzi,” alisema Shamata.
Hivyo alisema katika mpango huo Serikali kupitia wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi iendelee na dhamira yake ya utafutaji wa vifaa na kuwaendea wadau mbali mbali kuwaelezea dhamira ya Serikali vile ambavyo inakwenda katika kuimarisha pato la nchi yao.
Naye Mwakilishi wa jimbo la Kijini, Juma Makungu Juma, alisema katika upangaji wa upunguzaji wa kodi waangalie kima cha mshahara wa wafanyakazi wa chini.
Hivyo aliishauri Serikali wapendekeze mfanyakazi huyo kulipwa kulingana na masaa yake ambayo anayafanyia kazi au apunguziwe masaa hayo ya kazi ili kusudi aweze kupata nafasi ya kwenda kufanya kazi sehemu nyengine, vyenginevyo watakuwa wanawaumiza wananchi.