NA MWANAJUMA MMANGA

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Dk. Khalid Mohammed Salum amewataka wananchi kushajiika kulima mpunga kwa kutumia zana za kisasa ambazo zitaongeza tija.

Dk. Khalid alieleza hayo kwenye hafla ya uzinduzi wa uvunaji wa mpunga kwa kushirikiana na waziri wa Kilimo Umwagiliaji, Maliasili na  Mifugo, Dk. Soud Nahoda Hassan katika msimu huu wa mwaka 2020-2021 kwa wakulima wa kilimo cha umwagiliaji katika bonde la Cheju.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuwapa hamasa wakulima kuondokana na utegemezi wa mvua na badala yake kutumia kilimo cha umwagiliaji maji ambacho kinastahamili mabadiliko ya tabia nchi.

Aidha alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inachukua jitihada ya kuimarisha kilimo cha mpunga na kuwasaidia wakulima kwa kuwapatia zana za kilimo hicho ili kuondokana na utegemezi kwa wananchi na serikali.

Hivyo aliwaomba wakulima kujiunga katika jumuiya za wakulima ili kurahisisha utendaji kazi ambao unakuwa na tija kwa wakulima sambamba na kurahisisha kutatua changamoto zao zinazowakabili.

Pia aliwasisitiza kuhusu azma ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi juu ya suala zima la uchumi wa buluu kuwa ni muhimu sana.

Wakati huo huo Dk. Khalid alipata nafasi ya kutembelea na kukagua ofisi ya umoja wa wakulima na kukabidhi kompyuta na printa ili kurahisisha ufanyaji kazi katika ofisi ya jumuiya hiyo ya wakulima.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili, Mifugo na uvuvi, Dk. Soud Nahoda Hassan alisema wizara ya kilimo pamoja na kupiga hatua sekta hiyo Idara ya Umwagiliaji maji imeweza kutekeleza kilimo cha umwagiliaji maji kwa hatua kubwa na kufikia asilimia 98 ya utekelezaji wa huduma hiyo.

Hata hivyo idara inashirikiana na halmashauri za wilaya na mabaraza ya mji katika kusimamia jumuiya za wakulima wa umwagiliaji maji kwa ajili ya kuendeleza kilimo hicho.

Aidha Idara inaendelea kutoa taaluma ya kilimo bora cha umwagiliaji maji katika mabonde yote ya Unguja na Pemba, hivi sasa idara inasimamia na kufuatilia utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji maji inayotekelezwa katika mabonde saba ya kilimo hicho kwa Unguja na Pemba.

Miongoni mwa mabonde hayo ikiwemo Cheju, Kinyasini, Kibokwa, Kilombero na Chaani kwa Unguja na kwa Pemba bonde la Mlemele na Makwararani.

Alisema mradi huo ukimalizika utaendeleza jumla ya hekta 1,524 au ekari 3810, pamoja na miundombinu mengine mradi huo unajenga mabwawa manne katika bonde la Kinyasini, Chaani, Makwararani na Mlemele.

Alifahamisha kuwa mradi pia unachimba visima 49 kati ya hivyo 27 Cheju, vinane Kibokwa na 14 Kilombero.

Aliongeza kusema kuwa mradi huo unajenga misingi ya kuingiza na kutolea maji mashambani ambapo ushajenga misingi yenye urefu wa mita 23,200 katika mabonde ya Kinyasini na Kibokwa mpaka sasa imefikia asilimia 95 ya utekelezaji wake.

Nao wakulima wa eneo hilo wamepata nafasi ya kuishukuru Wizara ya Kilimo, Umwagiliaj,i Maliasili na Mifugo kwa kuendelea kuwathamini wakulima na kuiomba Wizara hiyo kuweza kutatua baadhi ya Changamoto za mitaro na zana bora za kilimo.