Yawataka wananchi kuchukua tahadhari

NA MADINA ISSA

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imetangaza tahadhari dhidi ya wimbi la tatu la maradhi ya corona na kuwataka wananchi kujiepusha na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima.

Akitangaza mkakati wa kujikinga na wimbi hilo waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Nassor Ahmed Mazrui, alisema serikali imeamua kutoa tahadhari hiyo kufuatia kuongezeka kwa ugonjwa huo katika baadhi ya nchi jirani na baadhi ya huduma kulazimika kusitishwa.

Alizitaja nchi ambazo zinakabiliwa na ongezeko la ugonjwa huo kuwa ni Uganda, DRC Congo na Afrika Kusini ambazo zina mafungamano na maingiliano ya watu wake hivyo hatua hiyo inaweza kusaidia Tanzania na wananchi wake kutopata madhara.

“Tunawaomba wananchi wajiepushe na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima, kuvaa barakoa, kunawa mikono pamoja na kujiepusha kushikana mikono kama njia ya kusalimiana,” alisema Mazrui.

Alisema licha ya nchi nyingi kuwa katika wimbi la tatu ya maradhi hayo, Zanzibar ipo salama kwa kuwa hakuna mtu aliyebainika kuwa na virusi vya maradhi hayo kati ya watu waliopita vituo vya uchunguzi kwa watu wanaoingia na kutoka Zanzibar, wakiwemo watalii na wageni kutoka nchi za nje.

Akizungumzia msimamo wa Zanzibar juu ya chanjo ya corona, Mazrui, alisema suala hilo ni la kitaifa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeunda kamati ya kitaalamu ya kufuatilia suala la chanjo kabla ya kutoa maamuzi kuhusu kutumika kwa chanjo hiyo ili kujiridhisha juu ya ubora na usalama wake.

“Baada ya kamati kumaliza kazi yake na chanjo ikathibitishwa kuanza kutumika, Mimi nitakua wa kwanza kuchanjwa ili kama ina madhara nianze kudhurika lakini suala hilo litafanyika kwa uwazi na wananchi wataarifiwa rasmi,” alisema Mazrui.

Hata hivyo, alifahamisha kuwa wakati kamati inaendelea kufanyia kazi majukumu waliyopewa, serikali ipo tayari kupokea chanjo ya aina yoyote ya Corona lakini haitoanza kutumika hadi Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakapotoa msimamo wa pamoja baada ya wataalamu kuwasilisha ripoti yao.

Aidha waziri Mazrui alizikumbusha taasisi zote na maeneo yanayotoa huduma kuzingatia kanuni na maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya juu ya suala la kujikinga na maambukizi ya corona katika maeneo yao ya kazi.

Kampeni ya kujihadhari na corona inaonekana kushuka kwa kiwango kikubwa tofauti na awali ulipoingia ugonjwa huo jambo ambalo linahitaji kuhamasishwa kwa nguvu na wataalamu wa afya pamoja na vyombo vya habari.