NA HAFSA GOLO

MWAKILISHI wa Jimbo la Mfenesini, Machano Othman Said amepongeza juhudi zinazochukuliwa na wajumbe wa kamati ya maendeleo shehia ya Kama katika utumiaji wa fursa za kuimarisha maendeleo na kuleta mageuzi ya uchumi ndani ya shehia hiyo.

Machano alieleza hayo katika mafunzo ya siku moja ya mikakati na  mpango wa maendeleo katika shehia ya Kama yaliofanyika katika skuli ya msingi Kama ambapo alisema shehia hiyo ina rasilimali  na fursa nyingi  zitazosaidia kuleta mageuzi  ya kiuchumi na kijamii.

Machano alizitaja miongoni mwa rasilimali hizo ni pamoja na eneo kubwa la ardhi, fukwe za bahari ,uwekezaji wa hoteli za kitalii, ili kusaidia  uchumi sambamba na kuibua miradi mengine ya maendeleo.

“Msifanye kazi kwa minongono au kuhutumiana miongoni mwenu kama mtaona mmoja wenu kakosea jambo la msingi ni kumuita katika vikao halali kumrekebisha haya mnayoyaona leo kama mngelikuwa mmeshayafanya mapema basi naamini shehia ya Kama ingepiga hatua kubwa ya maendeleo hata hivyo hatujachelewa jambo la msingi ni bidii na ari tutafikia malengo”,alisema.

Nae Katibu wa Shehia ya Kama Khamis Ali Khamis alisema, lengo la mafunzo hayo ni kuibua mwamko wa wananchi juu ya naendeleo na kuondokana na umasikini.

Sheha wa shehia ya Kama, Salum Said Seif, alisema bado  shehia hiyo yenye kaya 4,000 na 170 ni masikini, wajane 220 na watoto yatima zaidi ya 50, lakini wanakabiliwa na umasikini na wanashindwa kula milo mitatu kwa siku.

Nae, Mkufunzi, Amour Haji Yussuf, alisema viongozi hao wamepewa mafunzo ya kutambua fursa zilizomo ndani ya shehia hiyo, kutengeneza mpango  kazi wa maendeleo, kuondoa changamoto zinazoikabili shehia ya Kama  na mbinu za utatuzi wa migogoro.