Matumizi ya dawa za kulevya ni tatizo la kidunia
Tanzania ni muhanga wa mihadarati
Serikali zote mbili yajidhatiti kupambana na tatizo hilo
NA MOHAMMED SHARKSY (SUZA)
KILA ifikapo tarehe 26 Juni ya kila mwaka, Dunia inaadhimisha Siku ya Kupambana na Biashara na Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku hii kwa mwaka 2020 ni ‘Kauli mbiu ya mwaka huu ni Sema Ukweli juu ya Dawa za Kulevya Okoa maisha ya mwanadamu’ .Lengo ni kusaidia maboresho ya uelewa mpana zaidi wa mapambano dhidi ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya duniani.
HALI IKOJE KWA TANZANIA
Takribani watu milioni mbili wameathiriwa na madawa ya kulevya nchini, idadi hiyo ni kubwa sana ukilinganisha na Watanzania wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi nchini ambapo hali inaonesha kuwa ni watanzania 1,585,385 tu ndio huishi na VVU kwa sasa (kwa mujibu wa WHO).
Kwa mujibu wa makadirio yaliyofanyika mwaka 2014 kutokana na tafiti mbalimbali, Tanzania ilikadiriwa kuwa na watumiaji wa dawa za kulevya aina ya Heroin kati ya 250,000 hadi 420,500 na kati yao 30,000 wakitumia dawa hiyo kwa kujidunga (Consesus Estimate on Key Population Size and HIV Prevalence in Tanzania).
HALI IKOJE KWA ZANZIBAR
Zanzibar inakadiriwa kuwa na watu 10,000 wanaotumia Dawa za Kulevya, idadi hii imekuwa ikiongezeka siku hadi siku na kupelekea vitendo vya kihalifu kama unyang’anyaji, udhalilishaji, wizi na magonjwa mbali mbali kuongezeka katika jamii.
Hali hii imekuwa tishio kubwa kwa Afya, Usalama na Ustawi wa binadamu hasa kwa vijana na watu wazima.
Aidha, tatizo hili linachochewa sana na sababu kadhaa ikiwemo shindikizo rika, tamaa ya umiliki wa mali au utajiri wa haraka, malezi mabaya, kuvunjika kwa ndoa, kutokua na uwezo wa kujikwamua mtu kutokana na matatizo aliyonayo au msongo wa mawazo, kujiunga na marafiki wenye tabia mbaya.
Matumizi ya Dawa za Kulevya hasa hapa Zanzibar inachukuliwa kuwa ni njia ya mkato kwa baadhi ya vijana wanaotaka kupata utajiri wa haraka na badala yake kundi kubwa la vijana hao ndio watumiaji jambo ambalo linahatarisha na kudhoofisha nguvu kazi za taifa la baadae.
WATAALAMU WANASEMAJE?
Mamsab Ramadhani Mamsab, Muhadhiri kutoka Skuli ya Sayansi za Afya katika Chuo Kikuu Cha Taifa Cha Zanzibar (SUZA) akizungumza na makala haya nasema kuwa matumizi haramu ya dawa za kulevya yana madhara makubwa kwa afya, maisha na jamii katika ujumla wake.
Alizitaja changamoto ambazo huwakumba watumiaji wa dawa hizo kuwa ni pamoja na matatizo mbalimbali ya kiafya ikiwemo maambukizi mapya ya VVU.
Nae Daktari Huba Khamis Rashid wa SUZA alisema pamoja na kupungua kwa maambukizi mapya ya Virusi Vya UKIMWI, VVU, duniani kote, bado maambukizi miongoni mwa wanaotumia sindano za kujidunga madawa ya kulevya hayajapunguwa.
Hivyo, aliishauri jamii kuachana na matumizi ya dawa za kulevya ili kupunguza maradhi yangono yakiwemo hayo ya UKIMWI, kutokana na kujidunga sindano zisizo salama
Nae Abubakar Ameir Khamis, mwanafuzi wa mwaka wa tatu wa kada ya uuguzi kutoka Skuli ya Afya za Sayasi alisema vijana wengi hujiingiza katika matumizi ya madawa ya kulevya kwa kuhawishiwa na vijana waovu.
“Vijana ndio kila kitu, hivyo ukikumbana na vijana waovu ni rahisi sana kushawishika kama kulewa kuvuta bangi, madawa ya kulevya kutumia, kufanya ngono, n ahata wizi”, alisema.
WATENDAJI WANASEMAJE
Luteni Kanal Burhan Zubeir Nassor, ambae ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya alisema kuna changamoto kuhusu mwenendo wa kesi za dawa za kulevya mahakamani katika uendeshaji wa kesi hizo.
Alisema kwamba mara nyingi mwenendo wa kesi hizo hukumbwa na tatizo la baadhi ya mahakimu wa Mahakama kutokufata matakwa ya sheria ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya au kutovitumia baadhi ya vipengele vya Sheria hiyo vinavyowatia hatiani watuhumiwa wahalifu.
Aidha alisema kupewa adhabu ndogo kulingana na athari zinazopatikana katika jamii, tofauti na Tanzania Bara wanachukua hatua kali na kiasi kwamba mafanikio yao ni makubwa.
“Hali hii inapelekea kuzorotesha mwenendo mzima wa kesi za Dawa za Kulevya nchini, na kufanya watu kukosa imani na Mahakama”, alisema.
Aliitaja changamoto nyengine ni kwamba kutokuwepo siku maalum za kusikiliza kesi za Dawa za Kulevya ni tatizo jengine ambalo kwa namna moja au nyengine linaathiri mwenendo wa kesi hizo Mahkamani kutokana na baadhi ya Mahakimu wanaosimamia kesi za Dawa za Kulevya kuweka mbele maslahi binafsi kuliko maslahi ya Taifa.
Aliongeza kuwa ni lazima mahkama iweke mbele uzalendo katika kuendesha kesi za Dawa za Kulevya jambo ambalo litaleta taaswira nzuri kwa nchi lakini hata kwa jamii ambao ndio waathirika wakubwa.
Akitolea mfano kanuni ya 65 ya sheria ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya inayozungumzia viwango vidogo vidogo vya Dawa za kulevya imezuia dhamana kwa wale wote ambao wanakamatwa na viwango vikubwa vya Dawa za Kulevya ,Bangi kiwango kidogo ni 500 gms,Cocaine kiwango kidogo ni 1 gramu, Heroine kiwango kidogo ni gramu moja, Morphine kiwango kidogo ni 10 gms pamoja na Mirungi kiwango kidogo ni 500 gms.
Nae Mahamoud Ibrahim Mussa, Kaimu Mkurugenzi Kinga, Tiba na Marekibisho ya tabia kutoka Tume ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya alisema serikali ina nia njema ya kubadilisha sheria na kuhakikisha utekekeleaji wake,kusimamia utekelezaji wake na kuondosha muhali katika vita juu ya dawa za kulevya alisema.
WATUMIAJI WA DAWA ZA KULEVYA WANASEMAJE?
Mteja mmoja aliejitambulisha kwa jina la Ali ambae ni mteja wa dawa za kulevya kwa zaidi ya miaka 10 sasa, alisema aliinigia kwenye utumiaji wa madawa ya kulevya kutokana na Msongo wa mawazo.
“Hali hii iliweza kunipelekea hata nikaamua kutumia madawa ili niondokane na mawazo, lakini badala yake tatizo limekuwa kubwa, kwani lazima nipate kutumia”, alisema.
Mtumiaji mwengine wa madawa hayo aliejitambulisha kwa jina moja la Asha Mkaazi wa Miembeni alisema yeye aliingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya kutoka na ushawishi wa kujaribu jaribu, ili kuonja ladha yake kitendo kilichomfanya kufuata kama ni fasheni ya mjini ili asionekanena ushamba kwenye kundi la vijana wenzake.
Kama inavyoeleweka kuwa matumizi, biashara na usafirishaji wa dawa za kulevya ni tatizo la kidunia na kwamba kwa kiasi kikubwa linaathiri sana vijana wa nguvu kazi kwa taifa la sasa na baadae.
Hivyo, Zanzibar na Tanzania kwa ujumla zikiwa kama sehemu ya dunia kwa namna yoyote haziwezi kusalimika na janga hilo, nap engine ni kubwa zaidi ukilinganisha nan chi nyengine duniani.
Utumiaji wa dawa hizo huathiri nyanja zote zikiwemo afya, jamii, uchumi, siasa pamoja na ulinzi na usalama wa nchi yetu.
Kulingana na Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya Duniani ya mwaka 2017 inakadiriwa kuwa mwaka 2015 takribani watu wazima wapatao milioni 250 ambao ni sawa na asilimia 5 ya watu wote duniani walitumia dawa za kulevya na kati yao watu milioni 29.5 walipata matibabu kutokana na matumizi ya dawa hizo.
Dawa za kulevya pia zimekuwa zikiathiri afya kwa kuongeza maambukizi ya VVU, homa ya ini, kifua kikuu, magonjwa ya akili, utegemezi na mengine mengi.
TAFITI ZINAONESHA UKUBWA WA MADAWA YA KULEVYA NCHINI
Aidha Utafiti uliofanywa na Shirika la Kimataifa linaloshughulikia uchumi na Maendeleo “Organization for Economic Cooperation and Development” unaonyesha ikiwa dola bilioni moja zitokanazo na biashara ya dawa za kulevya zitatakaswa (kuwekezwa kwenye shughuli halali) basi uchumi hushuka kwa kiasi cha asilimia 0.03 hadi 0.06.
Matibabu stahili kwa watumiaji wa dawa za kulevya ni changamoto kwani takwimu zinaonyesha ni mraibu mmoja tu kati ya sita anayeweza kupatiwa matibabu kwa mwaka, Hali hii inatokana na ufinyu wa huduma za matibabu kwa waraibu.
Biashara ya dawa za kulevya hudhoofisha uchumi wa nchi, ukiangalia kwa haraka utafikiri kuwa fedha itokanayo na biashara ya dawa za kulevya inaongeza pato la ndani ya nchi, la hasha.
Fedha zinazotokana na biashara hiyo zinapochukua asilimia kubwa ya uchumi huongeza bei ya mali zisizohamishika, huvuruga biashara ya nje, huondoa ushindani kwenye biashara, huongeza tofauti ya vipato na kuongezeka kwa rushwa.
Kutokana na athari ya fedha hiyo kwenye mzunguko, wale wanaofanya kazi halali watashindwa kufanya baishara na kuondoka kwenye soko kwa kushindwa kushindana na wafanyabiashara wa dawa za kulevya.
Aidha matumizi ya dawa za kulevya huongeza mzigo kwa Taifa kwa kuwa hupunguza nguvu kazi na husababisha uharibifu wa mali.
Vilevile, gharama za udhibiti zikiwemo utoaji wa elimu kwa umma, uteketezaji wa mashamba ya bangi, uendeshaji wa kesi, kuwatunza wafungwa magerezani na kutibu uraibu na magonjwa yanayoambatana na utumiaji wa dawa za kulevya huongeza mzigo kwa taifa na jamii kwa ujumla.
Matokeo yake utawala wa sheria hautakuwepo, rushwa itatawala na hatimae fedha inayopatikana itatumika kuimarisha biashara ya dawa za kulevya.
Aidha bishara ya dawa za kulevya imetawaliwa na rushwa katika kila ngazi, Kwa mfano, katika ngazi ya uzalishaji, wakulima wa dawa za kulevya huweza kutoa rushwa kwa wanaotakiwa kuharibu mashamba yao na iwapo watakamatwa watatoa rushwa kwa polisi au majaji.
Vilevile, katika ngazi ya utengenezaji wa dawa za kulevya huweza kuwarubuni wafanyakazi wa viwanda vya kemikali bashirifu na inapofika ngazi ya usafirishaji wa dawa za kulevya, rushwa huweza kutolewa kwa wakaguzi wa mipakani kwa kutumia mianya iliyo katika sekta ya usafirishaji.
Kwa kutambua athari zinazosababishwa na tatizo hili, Serikali ya awamu ya tano ilipendekeza sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Nambari. 5 ya Mwaka 2015 ambayo ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuanza kutumika mwezi Septemba mwaka 2015.
Pamoja na kutunga sheria na jitihada zingine nchi yetu iliendelea kukabiliwa na biashara na matumizi ya dawa hizo
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la matumizi mabaya ya dawa tiba zenye asili ya kulevya ambazo ni Benzodiazepines, Ketamine, Tramadol na Pethidine.
Aidha, serikali imebaini kuwepo kwa uingizaji, utunzaji na utumiaji holela wa kemkali bashirifu unaoweza kusababisha uchepushaji wa kemikali hizo na kuweza kutengengeneza dawa za kulevya.
Kwa kutambua ukubwa wa athari zinazosababishwa na dawa za kulevya, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje imefanya jitihada mbalimbali za kukabiliana na tatizo hilo.
Jitihada hizo ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa taarifa za kiintelijensia, ukamataji wa wauzaji na wasambazaji wakubwa wa dawa hizo na kuwachukulia hatua wasiofuata taratibu za uingizaji, utunzaji, usambazaji na utumiaji wa kemikali bashirifu.
Hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kupambana na tatizo la dawa za kulevya kupitia wadau wake zimeleta matokeo chanya yakiwemo kukamatwa kwa kiasi kikubwa cha dawa za kulevya, kukamatwa kwa wasambazaji papa wa dawa hizo nchini na duniani kwa ujumla na kuongezeka kwa vituo vinavyotoa huduma kwa waraibu.
NAMNA SERIKALI INAVYOPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA
Katika kipindi cha mwaka 2017 Serikali imeimarisha udhibiti wa dawa za kulevya zinazopitia mipakani na kupunguza uingizaji wa dawa hizo nchini.
Hali hii inadhihirishwa na ongezeko la dawa za kulevya zilizokamatwa ikiwemo heroin ambayo katika mwaka 2016 ilikamatwa kilo 42.26 ikilinganishwa na kilo 185.557 zilizokamatwa mwaka 2017 ikiwa ni mara nne zaidi.
Takwimu zinaonesha kwamba kiasi cha bangi kilichokamatwa kimeshuka kutoka tani 68.23 kwa mwaka 2016 na kufikia tani 52.19 kwa mwaka 2017.
Taarifa ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya Mwaka 2017 inaeleza kuwa ukamataji wa mirungi uliongezeka kutoka tani 21.6 kwa mwaka 2016 hadi kufikia tani 67.8 kwa mwaka 2017 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya mara tatu.
Ongezeko hili limechangiwa na operesheni nyingi zilizofanyika katika kupambana na biashara ya mirungi ambapo idadi ya watuhumiwa waliokamatwa wakijihususha na mirungi ilipungua kutoka 2,397 kwa mwaka 2016 hadi kufikia 1,797 kwa mwaka 2017.
Aidha idadi ya watuhumiwa waliokamatwa wakijihusisha na bangi ilipungua kutoka 17,889 kwa mwaka 2016 hadi kufikia 11,528 kwa mwaka 2017.
Juhudi hizi za serikali zote mbili ni za kupongezwa hivyo wananchi ni vyema kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kuwafichua wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara ya madawa ya kulevya kwani Serikali ya viwanda itakuwa si lolote ikiwa nguvu kazi itateketea kwa ajili ya matumizi ya madawa ya kulevya.
Hata Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, alisema serikali imeamua kuunda tume ya kupambana na dawa hizo ili kuona linachukuliwa kwa ukubwa wake na kufanyiwa kazi.
Kwa pamoja tunaweza kufanikisha hili ikiwa kila mmoja atatimiza wajibu wake kwa nafasi aliyonayo.