NA MWANDISHI WETU
BAADA ya mapumziko waliopewa wachezaji, timu ya Simba imeanza mazoezi katika viwanja vya Mo Simba Arena vilivyopo Bunju jijini Dar es Salaam.
Wachezaji walipewa mapumziko ya siku nne baada ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Ruvu Shooting uliopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Juni 3 huku wale walioitwa timu zao za taifa wakiruhusiwa kwenda kujiunga nazo.
Kikosi kilichoanza mazoezi kinaundwa na wachezaji ambao hawajaitwa kwenye timu za taifa na wale walikuwa majeruhi na sasa wako fiti.
Mazoezi yatakuwa chini ya kocha wa viungo Adel Zrane ambaye atawarudisha katika hali ya kimichezo baada ya kutoka mapumziko.
Simba inatarajia kucheza mechi kadhaa za kirafiki ingawa bado hazijafamika kabla ya ligi kurejea, ambapo mchezo wa kwanza utakuwa dhidi ya Polisi Tanzania, Juni 19 katika uwanja wa CCM Kirumba.