NA LAYLAT KHALFAN

WIZARA ya Ardhi Maendeleo ya Makaazi, imesema ujenzi wa matofali utaongeza uharibifu wa mazingira na kuathiri kilimo katika maeneo tofauti ya visiwa vya Zanzibar.

Hayo yalielezwa na Waziri wa Wizara hiyo, Riziki Pembe Juma, wakati akijibu suala la Mwakilishi jimbo la Kojani, Hamad Hassan Omar, alietaka kujua serikali ina mpango gani wa kurejesha vituo vya kutengeneza matofali ya kuchoma ili kuwakomboa wananchi.

“Mhe Spika kwa mujibu wa wataalamu wa mazingira udongo ni miongoni mwa mali zisizorejesheka, hivyo serikali ikirihusu kuchimbwa udongo kwa ajili ya kutengenezwa matofali utaleta athari kubwa za kimazingira na kuathiri eneo la kilimo”, alisema Waziri huyo.

Alisema athari zinazotokana na mashimo ya uchimbaji udongo wa matofali itachukua muda mrefu kurejesha hali ya kawaida kurekebisha athari zake na ndio maana serikali inaona bado kuna umuhimu wa kutumia matofali ya mchanga na saruji.

Hata hivyo, alisema ni kweli matofali yanayotengenezwa kwa saruji na mchanga gharama yake ni kubwa ikilinganishwa na matofali ya udongo ya kuchomwa, lakini gharama za ujenzi kulingana na ukubwa wa nyumba kutoka kwa muhusika.

Aidha, Waziri Riziki alisema serikali haina mpango wa kurejesha vituo vya kutengeneza matofali ya kuchoma ya udongo kwasababu ya kuendelea kulinda uhifadhi na mazingira licha ya udongo wenye sifa zinazokubalika kuwa unapatikana katika eneo moja tu Zanzibar katika eneo la Kwarara, lakini eneo hilo hivi sasa limekuwa ni makaazi ya watu.

Hata hivyo alisema serikali itaendelea kujenga nyumba za gharama nafuu zikiwemo za ghorofa ili kuweka matumizi mazuri ya ardhi pamoja na kuendeleza sera ya serikali yakuwepatia makaazi bora wananchi wake.