NA MWAJUMA JUMA, KHAIRAT SULEIMAN

SERKALI ya  Mapinduzi Zanzibar, inakusudia kuwasaidia  wananchi kwa kuwapatia vyombo na mitego ya uvuvi, ili kuongeza kipato chao.

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi,  Abdalla Hussein Kombo, aliyasema hayo huko Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar, alipokua akijibu suala la Mwakilishi wa jimbo la Dimani, Mwanaasha Khamis Kombo, alietaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi hao,  ili kuongeza kipato na kunufaika na Uchumi wa Buluu.

Waziri Kombo, alisema mpango huo utafanyika kupitia utaratibu  wa Benki ambapo wananchi watapata fursa ya kupata mikopo itakayo wasaidia kuwekeza katika uvuvi.

Aidha, alisema mpango huo utakuwa ukifanyika  pale Serikali itakapopata fursa ya miradi ya maendeleo yenye kulenga huduma kama hiyo.

Sambamba na hayo alisema  Wizara itashirikiana na  wa wadau mbalimbali wa maendeleo katika kutafuta njia endelevu na mbadala za kuwasaidia wavuvi  boti na vifaa kwa ajili ya shughuli zao za uvuvi.

Hata hivyo, alisema kuwepo kwa mfuko Maalumu wa kuwasaidia wavuvi katika shughuli zao ni njia mojawapo ya kuwawezesha wavuvi hao kupata fedha za kuwekeza katika uvuvi.

Aidha alieleza kwamba kwa sasa wanawashajihisha wavuvi wadogo wadogo kujiunga na vikundi vya Ushirika vya Kuweka na kukopa (kwa mfano SACCOS) ili kurahisisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuwaongezea nguvu za kumudu  uvuvi wa kisasa.