NA MADINA ISSA

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema haitomfumbia macho wanaume ambao watashindwa kuwajibika kwa kutoa huduma kwa watoto baada ya wanandoa kuachana.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdallah, aliyasema hayo kwenye hotuba iliyosomwa na Waziri wa Nchi, Ofsi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Dk. Khalid Salum Mohamed, katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wajane Duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa ZSSF, Kariakoo.

Alisema, kumekuwa malalamiko mingi kutoka kwa wanawake waliochana nan a waume zao na Serikali itafuatilia kwa karibu malalamiko yote yanayohusiana na masuala hayo ili watakaokutwa na hatia wawe mfano kwa wengine.

Alisema, serikali inafahamu kwamba wako wanaume walioacha wake zao na watoto na hawawashughulikii kulingana na Sheria za nchi zinavyoelekeza.

Alisema kwa Zanzibar inaadhimisha siku hiyo kwa mara ya kwanza, hivyo ni vyema jamii kuwathamini mama wajane ili kuweza kupata haki zote za msingi ikiwemo kuheshimiwa na kupata haki zake zote za msingi ikiwemo kuheshimiwa na kulindwa.

Aidha, alifahamisha kuwa siku hii inalenga kuhakikisha watoto wa wajane wanaishi katika mazingira rafiki na salama kama walivyo watoto wengine ambao wanapata malezi ya baba na mama.

“Hii ina maana kwamba katika kuadhimisha siku hii basi jamii itambue kuwa mama mjane anapaswa kupata stahiki zake kwa mujibu wa Sheria bila ya pingamizi ya aina yoyote,” alisema.

Sambamba na hayo, Dk. Khalid alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Hussein Ali Mwinyi, imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha mama mjane wa Zanzibar anaishi kwa kuheshimiwa na kulindwa na kwamba anakuwa na uhuru na anapata haki zake zote za msingi.

“Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyi, alitoa mwelekeo wake katika kuhakikisha kuwa sheria zote kandamizi kwa mama mjane zinabadilishwa ili sasa mama wajane wawe kwenye mazingira mazuri kimaisha,” alieleza Hemed.

Alisema Serikali imekuwa ikichukua jitihada kubwa za kupinga na kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa aina zote ikiwemo wa wanawake na watoto hapa nchini.

Sambamba na hayo, kwa niaba ya Serikali, aliwapongeza viongozi wa Taasisi ya Kusaidia Wajane Zanzibar (ZAWIO) kwa moyo wao wa kujitolea kuhakikisha kuwa wanawake wajane wanapata haki zao kwa mujibu wa taratibu za nchi na kuhakikisha mama mjane anaishi katika mazingira yenye matumaini ambayo wengine wanaishi.

Pamoja na hayo, Makamu Hemed alisema takwimu zinaonesha kuwa kuna ongezeko kubwa la talaka katika jamii ambalo ndio chanzo cha ongezeko la wajane na kukosekana kwa malezi yaliyobora kwa watoto wetu.

Hivyo, aliitaka jamii kuwahimiza vijana wao wanaotarajia kufunga ndoa kushiriki mafunzo kabla ya ndoa yanayoendeshwa na Ofisi ya Mufti Zanzibar kwa ajili ya kuwatayarisha vyema vijana hao katika kuhimili maisha ya ndoa ili kuepukana na talaka zisizo na msingi.

Sambamba na hayo, alizitaka taasisi mbalimbali, mashirika binafsi, jumuiya za kitaifa na kimataifa, wafanyabiashara na wadau wengine kuiungana na Serikali ili iweze kuwasaidia kwa weledi mama wajane amba ni ukweli wamekuwa wanahitaji msaada mkubwa si tu kutoka kwa Serikali bali kila mmoja kwenye jamii.

Mapema Mkurugenzi wa Taasisi ya Kusaidia Wajane Zanzibar (ZAWIO), Tabia Makame Mohammed, aliwataka wanawake wajane kutokata tamaa badala yake kuendelea kupambana na kuzikabili changamoto zinazowakumba katika jamii.

Akisoma risala ya wanachama hao, Katibu wa taasisi hiyo, Khamis Ali Rashid, alisema lengo la kuundwa kwa jumuiya hiyo ni kumtetea, kumuwezesha, kumshirikisha na kumfanya mama mjane awe na thamani kama mwanamke na kama tegemeo kwa taifa badala ya kuwa tegemezi.

Aidha alisema kundi la mama wajane limeonekanwa kusahaulika jambo ambalo lilipelekkea kuanzishwa vyama, jumuiya na taasisi mbalimbali za kutetea na kusimaia Kwa biana ya wajane wote duniani.

Kauli mbiu ya siku ya wajane kwa mwaka huu inasema,“mapambano dhidi ya covid 19: wajane washiriki kikamilifu”.