NA MADINA ISSA

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema itaendelea kuchukua jitihada za kuhakikisha watoto wanapata haki zao na kuondokana na vitendo vya udhalilishaji.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Khamis Abdallah Said, alieleza hayo katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yaliyofanyika Kijiji cha kulelea watoto SOS kilichopo Mombasa Mjini Unguja.

Alisema ni vyema wazazi na walezi kuwawaptia haki watoto wote bila ya ubaguzi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanawapatia huduma bora za afya ikiwemo chanjo.

Alisema Idara ya Ustawi wa Jamii inasimamia maendeleo ya watoto na akina mama kwa kuwapatia haki zao na kupinga vitendo vya uzalilishaji vinavyowapata watoto.

Aidha alifahamisha kuwa changamoto kubwa zinazowapata watoto ni kutokupata haki zao za msingi, kudhaliliswa kijinsia, kutelekezwa na kutumikishwa kwenye ajira za utotoni jambo ambalo serikali inaendelea kulipiga vita ili kuona linaondoka nchini.

Nae, Mkurugenzi wa kijiji cha SOS, Asha Salim, alisema kuibuliwa vipaji vya watoto na kuviendeleza inawasaidia kuwapa umahiri katika kuimarisha vipaji vyao.

Alisema kuwapa haki na uhuru watoto, kunawajengea ujasiri na kuimarisha vipawa vyao hivyo kuna umuhimu jamii kulizingatia ja,mbo hilo.

Nao, watoto wa kijiji hicho, walipokuwa wakitoa ujumbe katika sherehe hiyo, walisema ni vyema kuhakikisha wanapata haki zao za kimsingi  ikiwemo malezi  na haki za mtoto kwani inaondosha changamoto zimazompata mtoto

 

Mapema, akifunga mdahalo kuadhimisha siku hiyo, Mkuu wa vijiji vya SOS Tanzania, David Mwalongo, aliitaka jamii kuwapatia watoto malezi bora ili wawe na makuzi bora lakini pia kuwakinga na vitendo viovu vinavyorudisha nyuma maendeleo yao.

“Watoto wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi katika jamii, ikiwemo kutoandaliwa mazingira mazuri ya maisha yao ya baadae, hivyo wazazi na jamii kwa jumla tunapaswa kuhakikisha tunawapatia haki zao za msingi ikiwemo elimu, afya na malezi bora,” alisema Mwalongo.

Akiwasilisha mada ya malezi bora, Mkuu wa Divisheni ya mtoto kutoka Idara ya jinsia na watoto, Mohammed Jabir Makame, alisema jamii inapaswa kuwa na malezi ya pamoja yatakayosaidia kuwa linda na vitendo vya udhalilishaji ambavyo vimeonekana kuongezeka nchini.

Nao watoto kutoka mabaraza ya watoto wa shehia za wilaya ya Magharibi ‘B’ waliviomba vyombo vya sheria kutoa adhabu kali kwa wahusika ambao kwa makusudi wana ongeza mbinu za kuharibu maisha yao.