Unaweza kumuathiri mlaji wa bidhaa iliyoathirika

NA ASHURA MWINYI

“KILIMO ni uti wa mgongo”, huu ni usemi maarufu ambao unatumiwa kwa ajili ya kuhamaisha kilimo na pia kutilia mkazo umuhimu wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi na maendeleo ya wananchi.

Maendeleo ya sayansi na teknolojia duniani yamegusa sehemu mbalimbali ikiwemo sekta ya kilimo, ambapo wataalamu hutumia sayansi na teknolojia ili kurahisisha shughuli za kilimo na kuongeza tija.

Pamoja na maendeleo ya sayansi na tekolojia katika kilimo, bado wakulima wetu hapa Zanzibar wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kwenye shughuli zao za kilimo, ikiwemo tatizo la ukungu (fungus).

Wataalamu wa kilimo hasa mabwana na mabibi shamba ni watu muhimu sana wanaopaswa kuwasaidia wakulima kuepukana na visababishi vya kuota ukungu (fungus).

Ukungu ama ‘fungus’, unaweza kujitokeza wakati wowote katika mazao na kwamba unaelezwa mazao ya chakula yenye ukungu yanaweza kumdhuru mtumiaji.

Hata hivyo wataalamu hao wanawahimiza wakulima kutumia njia bora za upandaji, uvunaji, usafirishaji na utunzaji wa mazao ya kilimo katika maghala ili kuepuka ukungu.

Wataalamu wanaeleza aina mbalimbali za sumu ambazo hujitokeza wakati wakulima wakiwa kwenye mataarisho ya kilimo, uvunaji na uhifadhi wa mazao kwenye ghala.

Mwandishi wa makala haya alifanya mahojiano na meneja mradi wa kudhibiti sumukuvu Zanzibar, kutoka wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Mwanaidi Ali Khatib ambae alielezea tatizo la sumukuvu ambayo inaweza kupatikana katika mazao yaliyoathiriwa na yaliyoshambuwa na ukungu.

Alisema sumukuvu ni kemikali zinazozalishwa na aina ya kuvu au ukungu (fangas) ambao wanaota kwenye punje za nafaka, mbegu za mafuta na unga wa nafaka.

Alisema kwamba aina za ukungu jamii ya ‘aspergillus’ wanaoota kwenye mazao mbalimbali ikiwemo nafaka na mbegu za mafuta, mikunde na mazao ya mizizi na kusababisha madhara kwa binaadamu na mifugo.

Meneja huyo alieleza kuwa sumukuvu huhatarisha afya ya mlaji na kuathiri uhakika wa chakula pamoja na kupunguza kipato cha mkulima.

Mwanaidi alieleza kwa upande wa uzalishaji sumukuvu inaweza kuanza shambani na kuendelea hadi katika uhifadhi wa mazo ya chakula hasa endapo mkulima hatokuwa makini na njia za kuepuka mazao yake kupata sumukuvu.

Alifafanua kuwa sumukuvu hupatikana zaidi katika mahindi na njugunyasa pamoja na bidhaa zinazotokana na mazao hayo. Mazao mengine ni pamoja na korosho, muhogo, alizeti, mtama na mchele.

Hata hivyo meneja huyo alisema uchafuzi katika mazao hutokea katika hatua yoyote ya mnyororo wa thamani kuanzia shambani kama mkulima hatofuata kanuni za kilimo bora kupanda kwa wakati maalum pamoja na ucheleweshwaji wa kuvuna kwa wakati kwa mazao yaliokomaa.

Meneja huyo alisema mikakati ya udhibiti imegawika katika njia mbili wakati wa uzalishaji na wakati wa uvunaji. “Hii ni muhimu kwa mkulima kuwa makini juu ya kudhibiti sumukuvu ili kuzuia uchafuzi katika hatua za mbeleni kama vile kufuata kanuni za kilimo bora”, alisema.

Mwanaid alisema mazao yapigwe?? vizuri kuepusha kupasuka, yakaushwe kwa hali ya ubora zaidi kufikia kwa asilimia ya unyevu kwa kiwango kinachokubalika kitaalamu na kuhifadhiwa.

Kwa upande wa uvunaji uangalizi mkubwa unahitajika katika kuvuna lazima mikakati itekelezwe ili kuweka mazingira bora ya uhifadhi pamoja na kudhibiti mashambulizi ya wadudu na fangasi.

Alieleza kuwa ni vyema kwa mkulima kutumia turubali, mikeka na majamvi kwa kuanika na kuepuka kuanika mazao chini ili kuepusha uchafuzi wa ukungu unaweza kuleta sumukuvu.

Alisema mazao kama njugu na mahindi lazima yahifadhiwe katika sehemu kavu na safi isiyo na joto litakalosababisha unyevunyevu katika chakula.

Meneja huyo aliwatahadharisha wakulima kuacha kuwapa wanyama kama kuku na ng’ombe chakula cha nafaka zilizooza au zilizoota ukungu kwani zina uwezekano mkubwa wa kuwa na sumukuvu na kusababisha madhara kwa mnyama pamoja na binaadamu atakaekula mazao yaliyotoka kwa mnyama aliyeathirika.

“Tokea shambani wakulima wanatakiwa kuyahifadhi mazao yao pia wavune kwa wakati pale mazao yanapokomaa”, alisema meneja huyo.

Nae Mwakilishi wa Mradi wa Kuzibiti Sumukuvu Zanzibar, Aisha Suleiman Mubandakazi alisema sumukuvu kiafya inaweza kusabaisha athari kwa binaadamu na mifugo ikiwa watakula mazao yenye kemikali hizo.

“Sumukuvu haionekani kwa macho, haina harufu wala ladha ila inaweza kutambuliwa kupitia kwa vipimo vya maabara”, alisema.

Alisema sumukuvu hasa zile za ‘aflatoxin’ zikiingia kwenye mfumo wa chakula haziwezi kuondolewa, hivyo ni lazima kuhakikisha sumu hizi zinadhibitiwa kabla hazijaingia katika mfumo wa chakula.

Vilevile sumukuvu inaweza kuzidisha ukali wa maradhi ya kuambukiza kama UKIMWI, kifua kikuu na homa ya ini pia unaweza kupoteza maisha endapo utakula chakula chenye sumukuvu kwa kiwango cha 1mg kwa kila kilogram moja.

Alibainisha kuwa sumukuvu hupatikana katika maziwa ya mama anaenyonyesha iwapo atakula chakula chenye sumu hiyo na pia husababisha kudhoofika kwa mwili na kudumaa kiakili kwa watoto wadogo chini ya umri wa miaka 5 ambao watakula chakula chenye sumukuvu.

Mwakilishi huyo alisema kwa upande wa Tanzania uchafuzi wa sumukuvu katika mazao uligundulika mnamo mwaka 2016 katika Mikoa ya Dodoma na Manyara kwa Tanzania ambapo baadhi ya watu waliugua na wengine walipoteza maisha kwa kula chakula kilichokuwa tayari kimeathirika na sumukuvu.

Hata hivyo alisema, madhara yanayoweza kutokea kwa muda mfupi baada ya kula chakula kilichokuwa na sumukuvu, kwa kiasi kikubwa ni pamoja na maumivu ya tumbo, kutapika na kuharisha, kuvimba tumbo, au miguu, homa na sehemu mbalimbali za mwili kama vile macho, ulimi, viganja, nyayoni na homa ya degedege.

Alisema madhara ya muda mrefu ya sumukuvu yanaweza kutokea baada ya mtu kula chakula kilichochafuliwa na sumukuvu kwa kiasi kidogo kwa muda mrefu kama vile saratani hasa ya ini, koo na figo na kushuka kwa kinga ya mwili.

Alifahamisha kuwa sumukuvu husababisha figo kushindwa kufanya kazi na kujitokeza kasoro kwenye mishipa ya fahamu na moyo na kuzidisha ukali wa maradhi ya kuambukiza.

Nae mwakilishi wa mradi wa kudhibiti sumukuvu Tanzania (TANIPAC), Ali Hamadi Ali kutoka Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, alisema sumukuvu inaweza kuporomoka bei za bidhaa katika soko dunia na kushindwa kusafirisha bidhaa nje.

“Umoja wa Ulaya umepunguza biashara ya mazao kutoka Afrika na kusababisha kupungua kwa hali ya uchumi katika biashara”, alisema.

Alisema kwa upande wa athari za kijamii, wananchi hukabiliwa na uhaba wa chakula na kupata njaa endapo sumukuvu itaathiri kwa kiwango kikubwa katika mazao.

Alisema Zanzibar katika mwaka wa 2020 kwa wafanyabiashara pamoja na viwanda ambavyo vinazalisha bidhaa za unga wa sembe viliingia hasara ya shilingi milioni 200 kutokana na mahindi kushambuliwa na sumukuvu.

Alisema baada ya kugundulika kwa tatizo la sumukuvu ofisa wa mradi huo walianza kutoa elimu kwa wakulima namna ya kuhifadhi na kuyafunika vizuri wakati wa kusafirisha mazao kwa ajili ya kuepuka upepea wa mvua usiingie katika mazao ili kuidhibiti sumukuvu kabla ya kumfikia mlaji.

Aliwataka wakulima kuyaweka mazao yao juu ya chanja yakiwa maghalani ili kupitisha hewa salama na kuacha kuweka kwenye sakafu moja kwa moja na kuepuka uotaji wa ukungu (fungus)kutokana na unyevunyevu.

Vyanzo vikuu vinavyosababisha uchafuzi wa sumukuvu alisema ni pamoja na uotaji wa ukungu unaotokana na hali ya joto kuwa kali kiasi cha kusababisha unyevunyevu katika sehemu ya kuhifadhia mazao.

Alifahamisha kuwa uotaji wa ukungu na kuzalishwa sumukuvu hutokea kwa kasi na kuenea kwa haraka hasa kukiwa na joto kali lenye nyuzi joto sentigredi 32 hadi 38 husababisha unyevunyevu katika hali ya hewa inayofikia asilimia 80-85.

Hata vivyo alisema mazao yapigwe vizuri kuepusha kupasuka, yakaushwe kwa hali ya ubora zaidi kufikia kwa asilimia ya unyevu kwa kiwango kinachokubalika kitaalamu.

Alisema uchafuzi wa sumukuvu huweza kutokea katika hatua yoyote ya mnyororo wa thamani yaani ni wakati wa kuvuna, usafirishaji, ukusanyaji na uhifadhi.

Wasimamizi wa mradi wa kudhibiti sumukuvu wameshauri kuchukuliwa tahadhari kuanzia kwa wakulima, wasambazaji, wafanyabiashara na kwa walaji kufuata maelekezo ya wataalamu.

Pamoja na hayo kutotumia njia bora za kilimo kuna uwezekano mkubwa wa kupotea kwa asilimia 90 ya chakula kutokana na kuingia sumukuvu katika mazao.

Vilevile waliwaomba wakulima kuchukuwa tahadhari tangu anapoliandaa shamba vizuri kwa kutumia mbegu zilizokomaa ili kupelekea kuota ukungu na kuzalisha sumukuvu.

Hata hivyo, wameinasihi jamii kwamba si kila ukungu ni sumukuvu na kuwaomba wakulima, wafanya biashara wawe waaminifu kwani usalama wa chakula unaanzia shambani, kwa mfanya biashara na mlaji.