NA TIMA SALEHE- DAR ES SALAAM

TIMU ya taifa ya Tanzania jana Juni 13 imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Malawi katika mchezo wa kirafiki uliochezwa Uwanja wa Mkapa.

Mchezo  ulikuwa na ushindani mkubwa kwa timu zote ambapo ilikuwa ngumu kipindi cha kwanza kwa ngome za timu zote kuokota mpira nyavuni.

Dakika ya 68 nahodha wa Stars, John Bocco alipachika bao la kwanza ambalo liliwanyanyua mashabiki kwa furaha.

Iliwachukua dakika saba  Stars kuandika bao la pili ambapo mtupiaji alikuwa ni Israel Patric ambaye alipiga pigo huru kiufundi likazama nyavuni na kumuacha kipa wa Malawi akiwa hana la kufanya.

Bao hilo lilifungwa dakika ya 75 baada ya Kibu Denis kufanyiwa madhambi nje kidogo ya 18, jambo ambalo liliwafanya Malawi washindwe kuwa na namna ya kupindua meza kwa dakika ambazo zilibaki.

Mpaka dakika 90 zinakamilika ubao wa Uwanja wa Mkapa ulikuwa unasoma kwamba Tanzania 2-0 Malawi.