NA VICTORIA GODFREY
UONGOZI wa Chama cha Mpira wa Wavu Tanzania (TAVA) umesema unaendelea kupambana, kuhakikisha timu ya Taifa ya wanaume ya Ufukweni inakwenda kushiriki mashindano ya Kombe la Afrika, ambayo yanatarajia kuanza kutimua vumbi Juni 21- 28 mwaka huu nchini Morocco.
Mashindano hayo ni muhimu kwa timu hiyo kwa ajili ya kutafuta nafasi ya kufuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki ya mwaka huu,itakayofanyika Tokyo, nchini Japan.
Aidha timu hiyo inatarajia kuondoka nchini Juni 19 mwaka huu,kuelekea katika kituo cha mashindano hayo yatakayoshirikisha mataifa mbalimbali ya Afrika.
Akizungumza na Zanzibarleo Mwenyekiti wa TAVA Meja Jenarali Mstaafu Patrick Mlowezi,alisema sasa maandalizi yamefikia kiwango cha 50/50 ya safari ya timu.
Alisema wanaendelea kuzungumza na wadau wa michezo mbalimbali kuhakikisha wanajitokeza kuunga mkono timu hiyo iweze kuipeperusha bendera ya Taifa.
“Hadi sasa uhakika wa kupeleka timu katika mashindano upo asilimia 50 ,lakini bado tunapambana kuhakikisha timu inakwenda,tunaomba wadau wa michezo waje watu wanaunga mkono ushindi wa timu ni wa Taifa zima,hivyo tuungane,” alisema Mlowezi.
Vikosi vinaundwa na timu mbili akiwemo David Neeke,Ford Edward na Ezekiel Rabson,Joseph Mafuru ambayo ipo chini ya kocha Mkuu Alfred Selengia.