NAJUMBE ISMAILLY, IGUNGA         

KUNDI la Tembo wanaokadiriwa kufika 800 wamevamia katika Kata ya Igoweko, wilayani Igunga, Mkoani Tabora na kisha kula hekari 66 za mazao ya chakula yakiwemo mahindi,mtama pamoja na mpunga na kusababisha kaya 50 za kata hiyo kukosa chakula.

Akitoa taarifa hizo kwenye mkutano wa Baraza la Madiwni wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Diwani wa Kata ya Igoweka, Omari Hamisi alifafanua kwamba kundi hilo la Tembo liliingia katika vitongoji viwili vya Igoweko “B” na Bugingija “D” na kula mazao ya wananchi waliokuwa hawajavuna na hivyo kusababisha kaya 50 kukosa chakula.

Kwa mujibu wa Hamisi kufuatia hali hiyo ndipo alipoiomba serikali kufika katika eneo hilo kwa ajili ya kuwatoa tembo hao ili wasiweze kuendelea kuleta madhara kwa wananchi sambamba na kuwalipa fidia  wananchi walioathirika.

Naye ofisa Maliasili wa wilaya ya Igunga, Jahulula Edward, alithibitisha kundi la tembo hao kuvamia makazi ya watu na kuharibu hekari 66 za mazao ya chakula na kwamba kati ya hekari hizo, hekari 42 ni za mahindi, hekri 17 ni za mtama na hekari saba ni za mpunga, lakini hakuweza kutaja thamani ya mazao yaliyoathiriwa na wanyama hao.

Hata hivyo, Edward alisisitiza kwamba tayari ameshawasiliana na Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Magharibi, ambacho kinatarajiwa kuwasili haraka katika eneo la Kata hiyo kwa ajili ya kuwaondoa tembo hao na kuwarudisha katika msitu wa Hifadhi wa  Unyambiu.

Aidha Ofisa maliasili huyo alisema kwamba idadi ya tembo imezidi ukubwa wa eneo la Hifadhi hiyo kutokana na wengi kutoka ndani ya Hifadhi na kuhatarisha usalama wa wananchi pamoja na mali zao.

Alifafanua Ofisa huyo wa maliasili kuwa msitu wa hifadhi wa Unyambiu wenye ukubwa usiopungua hekari 25, unakadiriwa kuwa na tembo  wasiopungua 800 na hivyo kutumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi kuwa makini na kuondokana na tabia ya kuwachokoza wanyama hao.

Edward hata hivyo alibainisha kuwa kaya nyingi zimejengwa karibu na eneo la hifadhi ambapo wanyama hao wanapotoka wamekuwa wakiingia kwenye makazi ya wananchi.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga, Pascrates Kweyamba alizitaja athari zilizowapata wananchi kutokana na uvamizi wa tembo hao kuwa ni pamoja na mazao ya kaya 50 yameliwa na wanyama hao.

Kwa mujibnu wa Mkurugenzi Kweyamba wanatarajia kufanya tathimini ya hasara iliyopatikana na kisha kupeleka kwenye Mamlaka husika kwa ajili ya malipo ya fidia.