TUNAPASWA kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kuwa salama dhidi ya janga la maradhi ya corona ambalo kwa sasa linaendelea kuwa tishio kubwa katika nchi mbalimbali duniani.

Zanzibar kama zilivyo nchi nyengine duniani ilikuwa miongoni mwa nchi ambazo baadhi ya watu walithibitika kuambukizwa ugonjwa wa corona mnamo mwezi Machi mwaka 2020.

Ugonjwa huo uliendelea kuishi nchini kwa miezi kadhaa hadi mwezi Juni ya mwaka 2020, ndipo corona ilipopungua na hatimaye kutoweka kwa kutokuwepo maambukizi.

Mnamo mwishoni mwa mwaka 2020 na mwanzoni mwa mwaka 2021, corona ilifumuka upya, hichi ndicho kipindi kilichoitwa wimbi la pili la ugonjwa wa corona, ambapo watu kadhaa waliugua na wengine kufariki dunia.

Hata hivyo msisitizo uliokuwa ukitolewa ni kuhakikisha wananchi wanachukua jitihada za kujikinga na maambukizi mapya na kusisitizwa kutumia tiba za asili.

Lakini alipoingia madarakani Rais wa awamu ya sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliunda tume maalum ya wataalamu iliyotafiti ugonjwa huo na kutoa ushauri serikalini namna ya kukabiliana nao.

Tume hiyo imekamilisha jukumu lake na imetoa mapendekezo takribana 19 kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano katika kukabiliana na ugonjwa huo hapa nchini.

Katika mapendekezo mengi yaliyopendekezwa na kamati hiyo ni tishio la Tanzania kupigwa na wimbi la tatu la ugonjwa wa corona, ambapo kwa mujibu wa taarifa rasmi tayari corona imesharudi rasmi.

Hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza na wahariri wa habari na waandishi wa habari ikulu jijini Dar es Salaam alisema Tanzania ina karibu wagonjwa 100 wa corona.

Bila shaka hili ndilo wimbi la tatu ambalo lilibashiriwa na wataalamu wa tume iliyoundwa na Rais Samia, ambapo katika baadhi ya nchi zilizopigwa na wimbi la tatu limeathiri vibaya sana.

Nchi kama Uganda na Kenya ambazo ni jirani na Tanzania, zinapitia kwenye wakati mgumu kutokana wimbi la tatu, ambapo limeingia rasmi Tanzania ambapo inaelezwa pia baadhi ya mikoa ya jirani nayo imeathirika.

Tunachoweza kusema ni kwamba serikali ya Jamhuri ya Muungano na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lazima zichukulie kwa makini tishio la wimbi la tatu la ugonjwa corona.

Mbali na serikali zetu, lakini jitihada kubwa katika kujikinga na corona ni jukumu la kila mwananchi hasa ikizingatiwa kuwa njia zote za maambukizi zinajulikana hivyo ni suala la utekelezaji.

Umefika wakati serikali kuingiza nchini chanjo ya ugonjwa huo, lakini lazima kazi ya kuzithibitisha chanjo zinazowafaa watanzania washirikishwe wataalamu wetu wa ndani.

Uchumi wetu unategemea utalii, hivyo tuhakikishe kila mwananchi anajilinda na kumlinda mwenziwe na tuwe makini na wageni wanaoingia kwa sababu jamii yetu ina tabia ya muhali.

Unapomkaribisha mgeni kutoka nje ya nchi hakikisha amepima na ana cheti kinachoonesha kuwa hana ugonjwa wa corona, inawezekana ukimficha corona itaanza na wewe.

Kuimarika kwa uchumi wetu hasa Zanzibar kutatokana na kustawi kwa utalii, lakini tukumbuke kuwa kustawi kwa utalii ni Zanzibar kutokuwa na corona.