Watajwa kuwa ni viongozi wa kimikakati

Hakuna linawashindalo pale wanapoamua

NA HAJI NASSOR, PEMBA

WANAWAKE na uongozi, wanawake wanaweza bila ya kuwezeshwa, wanawake ni majasiri, wanawake ndio wenye uchungu wa maendeleo.

Kauli hizi na nyengine zimekuwa maarufu sio Zanzibar pekee, lakini kila kona kama sio pembe ya ulimwengu huu wa karne ya 21.

Kila mmoja ni shahidi kuwa, kundi hili la wanawake liliachwa nyuma kwa karne nyingi za uhai zailizopita hapa ulimwenguni, likionekana kama vile halipaswi kufikia malengo yake.

Kwa Zanzibar wenye kukumbuka historia ya miaka kadhaa hadi mwaka 1964, pamoja na Zanzibar kutawaliwa na wakoloni na kuwepo kwa udhalilishaji, lakini wanawake walikuwa zaidi.

Inasemekana, walikuwa wakifanyishwa kazi kubwa yenye ujira mdogo, hawakuwa na nafasi ya kuuliza, kusikilizwa, kushiriki wala kushirikishwa, tena hata kwenye mambo yanayowahusu.

Lakini baada ya mwaka 1964 kwa Zanzibar kufanyika Mapinduzi ambayo yalikuja kumuondoa mkoloni, sasa alau wanawake kwa lugha za vijana wa sasa, wakaanza kupumua.

Ingawa, ilichukua muda sana kwa kundi hili la wazazi wetu kuonekana kama wana mchango ndani ya familia na taifa kwa ujumla, lakini walishasema wahenga kuwa papo kwa papo kamba hukata jiwe.

Ndani ya karne hii ya 21 sasa, baada ya wanawake kujikusanya kule Beijing nchini China mnamo mwaka 1995 na wakaibuka maazimio kadhaa, sasa hapo utetezi wa kupewa haki zao uliibuka.

Zama na kauli mbiu zilianza kuwa, wanawake wapewe haki zao, kisha wawezeshwe, wanawake wana haki ya uongozi, wengine wakaibuka kwamba wanawake na umiliki wa rasilimali kama vile ardhi.

Yote kwa yote hayo, ni ishara kwamba sasa kundi la wanawake ambalo kwa karne 20, lilikuwa limebanwa na makundi ya wanaume, sasa limeshaona bandari ya pale waendapo.

Lakini wapo viongozi kama vile aliyekuwa rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, wakati anaingia Ikulu ya Zanzibar mwaka 2010 na mwaka 2015 alianza kwa kuwapa nafasi za uwaziri.

Maana wengi walishaota mizizi kwenye akili zao kwamba, wanawake hawapaswi kuonekana kwenye meza refu wakiwa mawiziri au manaibu.

Kauli mbiu ya wanawake na uongozi wakati huo na sasa imeshikiliwa bango na wanaharakati kama vile Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania –TAMWA Zanzibar, ZAFELA, ZSLC, TGNP, ZAWCO na mradi wa WEZA III na ndio maana idadi ya wanaoibukia majimboni inaongezeka.

Kwa kisiwani Pemba kwenye uchaguzi wa kihistoria uliofanyika Oktoba 28 mwaka jana, kama vile ilikuwa na faraja kwa wanawake waliogembea kutimiza ndoto zao.