MOHAMMED ALI

MKUU wa mkoa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa, amesema kwamba atakuwa akifuatilia utekezaji wa utatuzi wa kero zinazotolewa na wananchi katika mikutano yake ndani ya shehia za mkoa huo.

Ametoa indhari hiyo katika mkutano wake na wananchi wa shehia ya Taveta, Meli nne, Kijitoupele na Uzi ulifanyika katika uwanja wa Magirisi, wilaya ya Maghribi ‘B’.

Alisema dhamira ya mikutano yake katika shehia sio tu kusikiliza kero hizo, bali kuhakikisha mamlaka zilizoachiwa kuzishughulikia zinafanya hivyo kwa muda waliopewa.

Kitwana aliutaka uongozi wa wilaya ya Magharibi ‘B’ na Masheha wa shehia hizo kuyapatia ufumbuzi malalamiko yaliyochini ya uwezo wao na kwa yale yaliyo nje ya mamlaka yao kuyafikisha mkoa ama sekta husika ili waweze kuyafanyia kazi.

Katika Mkutano huo, Kitwana aliwasisitiza wananchi kutowaficha watu wanaofanya vitendo ya uhalifu na udhalilishaji katika maeneo yao.

Aliongeza kuwa bila ya mashirikiano yao kazi ya kudhibiti vitendo ya vibaka, uhalifu na udalilishaji itakuwa vigumu kuweza kuidhibiti na kuwataka watoema shirikiano kwa serikali na vyombo vyake vya ulinzi katika kuyashughulikia mambo hayo.

Alieleza kwamba kwa upande mwengine mkoa kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi utaendelea na utaratibu wake wa kufanya doria na operesheni maalum katika maeneo yote ili kuimarisha amani katika mkoa huo.

Akiwa katika mkutano wake wa pili wa kukutana na wananchi, amesema kwamba amebaini baadhi ya taasisi zilizotakiwa ziwepo kwenye mikutano hiyo zimekuwa hazishiriki na kusababisha baadhi ya malalamiko ya wananchi kukosa majibu.

Katika mkutano huo Mkuu wa mkoa alimsimamisha kazi msimamizi wa kituo cha maji cha Kijitoupele kutokana na malalamiko ya wananchi wa Shehia hizo ya kukosa maji kwa muda mrefu licha ya utaratibu wa mgao wa maji uliowekwa na Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kwa shehia hizo.

Akijibu malalamiko ya wananchi kuhusu ubovu wa skuli ya msingi ya Mwanakwerekwe na uhaba wa madarasa skuli ya Msingi Tomondo, Mkuu wa Wilaya ya Magharibi, Hamida Mussa Khamis, alisema kwamba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali inatarajia kujenga skuli mpya za ghorofa na kuongeza majengo mengine katika skuli hizo.

Mbali na malalamiko ya ukosefu wa maji, skuli, barabara za ndani na malipo ya wazee, wananchi wa shehia ya hizo waliiomba pia serikali kuweka matuta katika barabara kuu eneo la Taveta kudhibiti ajali za mara kwa mara zinazotokea mahala hapo.

Aidha waliziomba kamati za mazingira za shehia kwa kushirikiana na mamlaka husika kudhibiti uchimbaji wa mchanga katika nguzo kubwa za umeme pamoja na kupatiwa dawa katika kituo cha afya magirisi.