NA MARYAM HASSAN
MKUU wa mkoa wa Kusini Unguja, Rashid Hadid Rashid, amesema ofisi yake itahakikisha inaendelea kushirikiana na wananchi katika kuimarisha huduma muhimu za kijamii.
Aliyasema hayo mara baada ya kufanya ziara ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Jumbi juu ya kilima hadi Chuo cha Utawala wa Umma (IPA).
Alisema serikali inatambua kwamba changamoto zilizopo hasa katika barabara za ndani ambazo zinazowakabili wakaazi hao.
Alisema wameweka mikakati ya kuziwekea lami barabara zote za ndani ili kuondosha usumbufu kwa wakaazi wa maeneo hayo na kuwataka kuendelea kuwa na subira.
“Niwahakikishie kuwa sasa serikali imeamua kuzijenga barabara za ndani zote hivyo nami nitasimama kidete kuhakikisha kila barabara itayojengwa inawekwa lami ili iwe imara zaidi,” alisema.
Naye Sheha wa shehia ya Jumbi, Muhidini Haji Machano, alisema watumiaji wa barabara hizo walikuwa wakipata usumbufu mkubwa hasa wakati wa mvua kutokana na ubovu hali inayopelekea madereva kushindwa kupeleka abiria hadi mwisho wa njia.
Alisema licha ya viongozi kuweka kifusi katika barabara hizo, bado wananchi walikuwa wanapata wakati mgumu kutokana na kuchimbika na muda mwengine kupelekea vyombo vya moto kuharibika.
“Hivi sasa barabara zimekuwa mbovu kweli kwa sababu ya mvua zilizonyesha zimepelekea kuharibika na nyengine kuwa na mashimo jambo ambalo hupelekea kutokea kwa ajali za mara kwa mara,” alisema Sheha huyo.
Kwa upande wao wakaazi wa shehia ya Jumbi wameushukuru uongozi wa mkoa huo pamoja na Kamati ya Maendeleo inayosimamia ujenzi wa barabara kwa hatua walizochukua.
Walisema kuanza ujenzi huo kwa hatua ya kutia kifusi na wameomba kuongezwa kasi zaidi ya ujenzi ili kumaliza haraka ili kuondokana na usumbufu wanaoupata.