NA LAYLAT KHALFAN

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, kwa miaka mingi imefanya jitihada za kurahisishia huduma muhimu wananchi wake ili kuwapunguzia ukali wa maisha.

Miongoni mwa jitihada hizo ni ujenzi au uimarishaji barabara za mjini na vijijini, huduma ya upatikanaji huduma za maji safi na salama, afya, elimu  ili kuona wananchi wanapata huduma muhimu zenye ustawi na kuondokana na changamoto zinazowakabili.

Hivi karibuni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohammed, alifungua barabara ya Pale – Kiongele iliyopo mkoa wa Kaskazini Unguja, kwa lengo la kuwekea mazingira mazuri wananchi wake.

Ufunguzi wa barabara hiyo ni kielelezo tosha cha kuwa nchi imefikia sehemu nzuri yenye matumaini makubwa ya upatikanaji maendeleo.

Hivyo ni vyema kwa watendaji waliokabidhiwa majukumu kuwa na wajibu mkubwa wa kulinda na kusimamia vyema matumizi ya fedha pamoja na kulinda miundombinu inayoanzishwa na serikali ili kudumu kwa muda mrefu.

Dhamira ya serikali ya awamu ya nane ni kuwatumikia wananchi kwa lengo la kuwakomboa na hali ngumu ya umaskini na kurahisisha huduma muhimu ikiwemo ya usafiri.

Hapo kale wazee wetu walishindwa walikuwa na maisha magumu kutokana na mateso waliyokuwa wakiyapata kutoka kwa watawala wa nchi hii ambao walitumia udhaifu huo kuwanyonya bila ya chembe ya huruma.

Muda mwingi walikuwa wanatembea masafa marefu kwa miguu kiasi ambacho miundombinu waliyokuwa wakiyatumia haikustahiki kwa binadamu wa kawaida.

Kwa sasa wananchi wa Zanzibar wanapata huduma hiyo kwa urahisi jambo linalowapa kila sababu ya kuipenda na kuithamini serikali yao.

Bila shaka ni haki ya kila mmoja miongoni mwao kuishukuru na kuiwapongeza viongozi wa serikai kwa kutekeleza mipango inayowapa unafuu katika maisha yao ya kila siku.

Ni ukweli uliowazi kwamba ujenzi wa barabara hiyo ni miongoni kazi za utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ile ya 2015/2020 ambayo iliahidi kujenga ustawi wa wananchi kwa kuwapatia huduma muhimu na kuwaondolea adha zilizokua zikiwakabili.

Hivyo ili barabara hiyo idumu na iendelee kutumika siku hadi siku ni vyema serikali kuwaajiri vijana ili waweze kuwa na usimamizi mzuri wa kuifanyia matunzo ya usafi  ili ionekane  muonekano ulio bora.

Mara nyingi tumekuwa tukishuhudia barabara za mjini na vijijini kutokuwa na taswira njema kiasi cha kundoa uhalisia wake kutokana na uchafu au kutodumu kwa muda mrefu.

Tunatambua Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kwa ajili ya kuweka mazingira ya miundombinu hiyo imara lakini kuna baadhi ya watendaji wanashindwa kutekeleza wajibu wao kikamilifu na kupelekea kuharibika kwa miundombinu hiyo katika muda mfupi.

Imefika wakatoi basi wajenzi na taasisi inayohusika na ujenzi wa barabara kuhakikisha wanazijenga barabara hizo kwa kuzingatia viwango na ubora wa hali ya juu na kujiepusha na michezo michafu ikiwemo ya kutofuata taratibu za ujenzi.

Hali hiyo kamwe haitotufikisha mahali kwani seriklai itakuwa inaelekeza nguvu kubwa kwenye ujenzi wa miundombinu hiyo lakini kutokana na kujengwa chini ya ubora, hulazimika kujenga tena katika kipindi kifupi.

Kwa hakika miradi inayojengwa maeneo mbali mbali nchi ukiwemo wa barabara hiyo ni jambo la kujivunia kwa wananchi wa kijiji hicho kwani utaweza kuondoa usumbufu wa muda mrefu kwa wenyeji na wageni watakao tumia njia hiyo.

Kwa mnasaba huo ni vyema wananchi wa maeneo hayo kushirikiana na serikali kuitunza barabara hiyo lakini pia kuwafichua watu wanaohujumu ujenzi wa miradi kama hiyo ili nchi ipate maendeleo yatakayowanufaisha wote.