NA ABUBAKARI AKIDA, ARUSHA

IDARA ya Uhamiaji imetakiwa kuongeza kasi, kulinda na kuwa na uadilifu katika ukusanyaji wa mapato yanayotokana na shughuli za uhamiaji ili kuweza kulisaidia Taifa katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo, wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli mbali mbali katika Kituo cha Namanga, ikiwa ni kukagua maeneo yanayotumika kwa uingiaji , utokaji wa wageni na wenyeji  lengo ikiwa kudhibiti wimbi la wahamiaji haramu wanaokamatwa mikoa mbalimbali nchini.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia anawategemea sana, kwanza katika ulinzi wa nchi, ulinzi wa raia na mali zao, ikifika sehemu tukasema Tanzania ina amani basi nyie askari wetu ndio mmefanya kazi hiyo, mnalinda mipaka yetu usiku na mchana” alisema

Alisema Rais Samia anawategemea uhamiaji katika ukusanyaji wa mapato, na wahakikishe mapato yote yanayotokana na shughuli za kiuhamiaji kuyadhibiti ili yatumike katika kujenga Taifa hili, jiepusheni na rushwa.

Pia aliwataka askari hao kuongeza kasi ya misako na doria kwa usalama wa nchi ili wananchi waweze kushiriki shughuli zao za kimaendeleo kwa amani na salama ikiwa ni adhma ya serikali kuona wananchi wanafanya shughuli zao kwa amani na usalama.

Akisoma taarifa mbele ya Naibu Waziri, Afisa Uhamiaji Mfawidhi wa Kituo cha Namanga, Mrakibu wa Uhamiaji, Prolimina Tairo amesema  kumekuwepo kushuka kwa mapato kulikosababishwa na janga la Korona ambako idadi ya wageni wanaoingia nchini imeshuka.

“Kuanzia mwezi Januari mpaka Mei Idara ya Uhamiaji katika Kituo cha Namanga tumekusanya jumla ya Dola za Kimarekani 180,780 tofauti mwaka jana kipindi kama hiki tulikua tumekusanya Dola za Kimarekani 450,000 na kushuka huko kunasababishwa na janga la Korona ambalo linaathiri shughuli za uingaiji na utokaji kutokana na vizuizi vilivyowekwa kwa raia wa nchi mbalimbali wanaopitia katika mpaka huu wa Namanga” alisema Tairo

Jumla ya wahamiaji haramu 11 wamekamatwa katika Wilaya ya Longido wakati wa operesheni ya kukamata wahamiaji inayoendelea katika mikoa yote iliyopo mpakani mwa Tanzania na nchi Jirani.