Miaka michache ijayo tembo kutoweka
TANGU enzi na dahari Afrika imekuwa eneo muhimu sana katika uzalishaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda vya sehemu nyengine duniani hasa barani Ulaya.
Maendeleo ya viwanda yaliyostawisha bara la Ulaya hadi kuwa na nchi zilizoendelea hasa katika karne ya 18, 19 na 20, malighafi nyingi za viwanda hivyo zilitoka Afrika.
Mataifa ya magharibi baada ya kunogewa na rasilimali za Afrika, ndipo yalipoamua kuzitawala ili wafaidi zaidi uvunaji wa malighafi katika bara hili zitakazoweza kuongeza uzalishaji kwenye viwanda vyao.
Mataifa hayo wakati yanazitawala nchi za kiafrika walivuna mamilioni ya tani ya madini zikiwemo dhahabu, almasi, mazao ya kilimo kama vile pamba, tumbaku na hata mazao ya chakula na matunda.
Kwa jinsi wazungu walivyokuwa wabaya, walichukua malighafi kwa njia ya uporaji ama kuzinunua kwa bei poa, lakini walikuja kutuuzia sisi wenyewe bidhaa zilizotokana na malighafi hizo kwa bei ya juu.
Hata baada ya ukoloni kutoweka, bara la Afrika limekuwa sawa na ile nyimbo tuliyokuwa tukiimba zamani wakati huo tukiwa watoto ‘al-fola’ al-fola’, ‘al-fola’ imekufa imebakia mafupa.
Kwa jinsi mataifa ya Ulaya yalivyomong’onyoa na kudhoofisha uchumi wa bara hili, takriban zaidi ya asilimia 95 ya nchi zake zimekuwa tegemezi kutokana na kutojimu kiuchumi ujenzi wa miundombinu na hata usambazaji wa huduma za jamii.
Moja katika uporaji wa malighafi zinazokwenda ng’ambu hadi hivi sasa ni meno ya tembo yanayotokana na wimbi kubwa la ujangili linaloendelea kufanywa kila uchao barani Afrika.
Tatizo hili limekuwa baya sana barani Afrika na kwa kiasi linatishia kutoweka kwa wanyama aina ya tembo na vifaru ambao pembe zao zimekuwa dili kubwa huko duniani.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa unaonyesha kuwa idadi ya tembo barani Afrika inazidi kupungua kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya ujangili ambavyo vimewaangamiza tembo zaidi ya 140,000 kati ya mwaka 2007 na 2014.
Ripoti iliyochapishwa hivi karibuni na jarida la Peer J, imeeleza kuwa utafiti uliobainisha kupotea maisha ya tembo hao umefanywa zaidi katika ukanda wa savana.
Eneo hilo ni rahisi kufanywa utafiti wa tembo kutokana na urahisi wa kuonekana wanyama hao ikilinganishwa na tembo walioko porini na umeonyesha kuwa idadi ya tembo inazidi kutoweka huku sababu kubwa ikiwa ni ujangili.
Utafiti huo ulibainisha kuwa ujangili ni miongoni mwa makosa ya jinai makongwe barani Afrika kutokana na kufanywa siku nyingi, lakini ulishamiri zaidi kuanzia mwaka 2005 na kusababisha maisha zaidi ya tembo 30,000 kupotea mwaka 2017.
Inakadiriwa kuwa idadi ya tembo walio katika ukanda wa savana katika nchi 18 ni 352,271 ambayo ni asilimia 93 ya tembo wote katika nchi hizo pamoja na kuwa utafiti huo.