BERLIN, UJERUMANI

UJERUMANI imewaondoa wanajeshi wake wa mwisho kutoka Afghanistan, na kuhitimisha operesheni zake za kijeshi katika taifa hilo.

Wanajeshi wa mwisho wa Ujerumani katika ujumbe wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO walisafirishwa kwa ndege kutoka kambi ya Mazar-i-Sharif na jeshi la anga la Ujerumani jana, na kuukamilisha ujumhe wake ambao ulianza karibu miaka 20 iliyopita.

Waziri wa Ulinzi Annegret Kramp-Karrenbauer amesema ukurasa wa kihistoria umekamilika katika operesheni kali iliyolipa changamoto jeshi la Ujerumani – Bundeswehr, na ambapo jeshi hilo limedhihirisha umahiri wake katika vita vya Afghanistan.

Kwa mujibu wa Bundeswehr, wanajeshi 59 waliuawa wakati wa operesheni hiyo, wakiwemo 35 katika mashambulizi au vitani.

Aidha Kramp-Karrenbauer amesema Ujerumani inawapa hifadhi wanajeshi wa Afghanistan waliowasaidia Wajerumani kwa mfano wakalimani.