NEW YORK, UMOJA WA MATAIFA
BARAZA la Usalama la Umoja wa Mataifa limeamua kuongeza muda kwa mwaka mwingine mfululizo wa idhini kwa nchi wanachama kukagua vyombo kwenye bahari kuu katika pwani ya Libya kwa wanaoshukiwa kukiuka vikwazo vya silaha.
Kwa pamoja walipitisha Azimio nambari 2578 (2021) chini ya Sura ya VII ya Hati ya Umoja wa Mataifa, chombo ambapo kiliwashirikisha wanachama 15 kiliamua kuongeza idhini zilizowekwa katika Azimio la 2526 (2020) kwa miezi 12 zaidi.
Hatua hizo zilizokubaliwa kwa mara ya kwanza katika Azimio la 2292 (2016) – huruhusu mataifa, yanayofanya kazi kitaifa au kupitia mashirika ya kieneo, kukagua vyombo kwenye bahari kuu zilizokwenda au kutoka Libya, ikipewa sababu nzuri za kuamini kwamba zinakiuka marufuku ya silaha ya Baraza la umoja wa mataifa.
Katika hatua nyengine, wanachama hao walimtaka katibu mkuu kuripoti juu ya utekelezaji wa azimio hilo la juzi la Alhamisi ndani ya miezi 11.
Baraza la Usalama liliweka vikwazo, pamoja na marufuku ya silaha, kwa Libya mnamo mwaka 2011 baada ya machafuko ya kisiasa ambayo yalisababisha kuangushwa kwa kiongozi wa zamani Muammar Gaddafi.
Mnamo Juni mwaka 2016, Baraza lilipitisha azimio la kuidhinisha ukaguzi wa vyombo kwenye bahari kuu sambamba na kutekeleza zuio la silaha ambapo kwa sasa katazo hilo limeongezwa muda na baraza hilo.