NA ALI SHAABAN JUMA
KUNA mambo mengi ya kipekee duniani ambayo wengi wetu hatuyajui. Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na yale ya kimaumbile, kihistoria, sanaa na utamaduni, watu na mataifa mbalimbali.
Wengi tumesoma jiografia na kujua mengi kuhusu maumbile ya duniani, lakini ni wachache miongoni mwetu ambao tunafahamu ni eneo gani la bahari lenye kina kirefu cha maji duniani.
Eneo la bahari lenye kina kirefu cha maji duniani ni mlango wa bahari uitwao Mariana Trench uliyoko katika bahari ya Pasifiki. Kina cha maji cha eneo hilo ni mita 11,034 masafa ambayo ni sawa na maili saba.
Nchi ambayo iko mbali kabisa ulimwenguni ni visiwa vya Tristan da Cunha vilivyopo kusini mwa bahari kuu ya Atlantiki. Visiwa hivyo viko umbali wa kilomita 2,434 kutoka visiwa vya Saint Helena ambayo ndivyo eneo la karibu linaloishi binaadamu.
Mto mrefu kabisa duniani ni Mto Nile wenye urefu wa kilomita 6,853 ambapo maji ya mto huo yanatumiwa na zaidi ya watu milioni 300 wa mataifa 11. Mataifa hayo ni Ethiopia, Sudan, Sudan ya Kusini, Misri, Rwanda, Tanzania, Uganda, Burundi, Congo DRC pamoja na Eritrea.
Ziwa lenye kina kirefu cha maji ulimwenguni ni Ziwa Baikal lilioko huko Siberia ambalo lina kina cha maji cha urefu wa mita 1,620.
Huko nchini Misri kuna piramid 100 moja katika mji wa Giza ambayo ni moja kati ya maajabu saba ya duniani. Piramid zimengwa kama makaburi ya mtawala wa Misri wa wakati huo aitwae Firauni wa pili katika karne ya 26 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa.
Piramid zilijengwa kwa muda wa miaka 27. Mawe makubwa mithili ya matofali yaliyochongwa na kujengewa piramid hizo kila moja lina uzito wa tani 2.5 ambapo kuna matofali ya aina hiyo milioni 2.3.
Ukuta Mkuu wa China ambao maarufu kwa jina la “The Great Wall of China” ulianza kujengwa mwaka 221 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa baada ya aliyekuwa mtawala wa China wakati huo aitwae Quin Shi Huang kuamrisha ujenzi wa ukuta huo ambao ulimalizika katika mwaka 1878 wakati wa utawala wa Quing.
Sehemu kubwa ya ukuta huo ambao unaonekana hivi sasa ulijengwa wakati wa utawala wa Ming karibu miaka 600 iliyopita. Vibarua wengi waliojenga ukuta huo ni askari na wahalifu ambapo inasemekana kuwa zaidi ya vibarua 400,000 walikufa wakati wa ujenzi huo. Watu hao walizikwa pembeni ya ukuta huo.
Ukuta huo una urefu wa maili 5,000 na katika hali ya kawaida mtu itamchukua miezi 18 kwa mwendo wa miguu kuanzia mwanzo hadi mwisho wa ukuta huo.
Nchi ambayo bendera yake ina rangi nyingi duniani ni Belize ambayo bendera yake ina jumla ya rangi 12. Baadhi ya rangi hizo ni buluu, nyekundu, nyeupe, kijani, manjano, udongo na nyeusi.