Michezo mengine yaingia nusu fainali

NA AMEIR KHALID, MTWARA

TIMU ya mpira wa Meza ya wanawake imetwaa ubingwa wa mashindano ya Umisseta baada ya kuwafunga mkoa wa Njombe seti 3 – 1.

Katika hatua ya nusu fainali timu hiyo imewafunga mkoa wa Iringa kwa seti 3 – 0 ambapo kwa upande wa wanaume timu hiyo imepata nafasi ya tatu baada ya kuwafunga mkoa wa Ruvuma seti 3 – 0.

Aidha timu ya mpira wa mikono wanaume imefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali baada ya kuwafunga mkoa wa Geita mabao 38 – 11 huku wanawake wakiingia nusu fainali baada ya ushindi wa mabao 20 – 11 dhidi ya mkoa wa Tabora, mchezo ambao ulikuwa mgumu kutokana na ushindani uliooneshwa na Tabora hasa kipindi cha pili.

Kwa upande wa mpira wa wavu Unguja imetinga nusu fainali baada ya kushinda 3 – 2 dhidi ya wenyeji Mtwara, pambano ambalo lilikuwa ngumu kwani Unguja walianza kwa kufungwa na kufanya kazi ya ziada kurejesha na kuongeza seti nyingine.

Katika mchezo wa mpira wa miguu kanda ya Pemba imeingia nusu fainali baada ya kushinda kwa penalti 5 – 4 dhidi ya mkoa wa Njombe huku golikipa wa Pemba, Ali Juma Mohammed, aliibuka shiujaa baada ya kupangua penalti moja na kuipa ushindi timu yake.

Kwenye riadha jana kanda ya Unguja imefanikiwa kupata medali nyingine mbili za dhahabu moja kwa mbio za kupekezana vijiti baada kwa kupata nafasi ya kwanza na medali ya shaba katika mbio za mita 100 wanaume.