NA MARYAM HASSAN

UPANDE wa mashitaka wa serikali, umepinga kuondolewa shitaka linalomkabili mshitakiwa Abdalla Khatib Vuai maarufu Mmuyuni (30) mkaazi wa Unguja Ukuu, aliyetuhumiwa kutenda kosa la wizi wa Mifugo.

Pingamizi hizi zimetolewa na Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Ayoub Nassor, baada ya mshitakiwa kuomba kuondolewa shitaka lake kwa kuwa ni la muda mrefu.

Wakili huyo alieleza kuwa, upande wao mwezi uliopita waliwasilisha shahidi, hivyo hakuna haja ya kuondolewa shauri hilo kwa kuwa bado wanao uwezo wa kuwaleta mashahidi.

Alisema, kilichokwamisha kufika shahidi katika kikao hicho ni kuwa, shahidi waliyemtegemea amepatwa na dharura.

Hivyo aliiomba mahakama kuahirisha shauri hilo na kupanga tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa ushahidi.

Maelezo hayo aliyatoa mbele ya Hakimu wa mahakama ya mkoa Mwera Said Hemed Khalfan, ambae aliridhia ombi la wakili huyo.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 15 mwaka huu kwa ajili ya kuskilizwa ushahidi, huku akiamuru kuwa amri zilizotolewa zibaki kama zilivyo.

Mshitakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Julai 26 mwaka 2019 baina ya saa 6:00 mchana hadi saa 8:00 mchana, huko Chimbe chimbe wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.

Bila ya halali na kwa makusudi, aliiba ngo’mbe mmoja dume mwenye rangi nyekundu kwa weupe mwenye thamani ya shilingi 800,000 kwa kukisia, mali ya Farudu Mohammed Bakari, jambo ambalo ni kosa kisheria.