NA JOSEPH NGILISHO,BABATI

UPELELEZI wa Kesi ya kushikwa  na dawa za kulevya aina ya Mirungi inayomkabili Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Saut tawi la Arusha, Subilaga Masebo (50) Mkazi wa Ngarenaro Jijini Arusha  na wenzake wanne umekamilika.

Kesi hiyo namba 39/2021 inasikilizwa na hakimu wa mahakama ya wilaya ya Babati Mkoani Manyara, Victa Kimario, ilikuja mahakamani hapo Jana kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Hata hivyo iliahirishwa baada ya mshtakiwa namba tatu, Hemed Hamad au Nyokaa (33) kutofika mahakamani kwa sababu ya kuugua akiwa gerezani.

Washtakiwa wengine ni, Hilary Mmbando (28) mkazi wa Komoto ,Babati, Ramadhani Hasan (33) Mkazi wa majengo ya zamani ,Babati na Ally Juma (53) Mkazi wa Majengo Babati

Akiongea mbele ya Hakimu, Kimario , mwanasheria wa Serikali, Lucian Shaaban, aliieleza mahakama hiyo kwamba shauri hilo lilikuja mahakamani hapo kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali baada ya upelelezi kukamilika .

Alfahamisha mshtakiwa namba tatu ,Hemed Hamadi ameshindwa kufika mahakamani baada ya kuugua akiwa gerezani na hivyo kuiomba mahakama tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na shauri hilo.

Wakili wa upande wa utetezi , Kapimpiti Mgalula anayemwakilisha mshtakiwa wa kwanza, Subilaga Masebo katika Kesi hiyo,  alisema kuwa hana pingamizi juu ya hoja hiyo ndipo hakimu Kimario alipoahirisha shauri hilo hadi Julai 2, 2021 ambapo Kesi hiyo itakuja kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Washtakiwa wote kwa pamoja walirejeshwa mahabusu katika gereza kuu la Babati Mkoani Manyara, kutokana na Kesi hiyo ya jinai kutokuwa na dhamana kisheria.

Awali washtakiwa hao wakiongozwa na mshtakiwa namba moja Subilaga Masebo,walikamatwa na Mirungi kilo 49.50 ikiwa kwenye gari na baadaye kufikishwa katika mahakama hiyo April 29 ,2021.