HAKUNA anayebisha kwamba vyombo vya usafiri yakiwemo magari ni sehemu ya maendeleo katika nchi yoyote ile.

Bila shaka usafiri wa gari kwa nchi ni muhimu kwani hurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii zifanyike kwa ufanisi na haraka.

Kwa muktadha huo, ndio maana sasa wananchi wengi wamejiendeleza kiuchumi na kumudu kujinunulia magari ya kutembelea pamoja na ya kufanyia biashara.

Katika miaka ya karibuni ambapo Zanzibar imekuwa ikiendesha mfumo wa biashara huria, kumeshuhudiwa kasi kubwa ya ongezeko la gari, hata hivyo badala ya ongezeko hilo kuleta faraja na raha, sasa imekuwa ni usumbufu na karaha.

Hali hii inatokana na ukweli kwamba mji wetu mkuu Zanzibar ni mmoja tu na tayari umekuwa mdogo kwani wananchi wengi ndiko wanakofanyia shughuli zao za kuendesha maisha ikiwemo biashara.

Ingawa siku hizi kumechipuka miji mipya pembezoni mwa Mji Mkongwe wa Zanzibar ikiwemo Mombasa kwa Mchina, Mwanakwerekwe, Bububu, Kisauni na sasa tunaelekea Tunguu, Mbweni na Fumba, bado mji wa Zanzibar unabaki kuwa mji tegemeo.

Kwa sababu hii, licha ya nyumba nyingi za makaazi kujengwa nje ya manispaa ya Zanzibar na watu kuhamia huko, lakini ifikapo asubuhi mji huo unakuwa hautoshi kwani asilimia kubwa ya wananchi wanaofanya kazi mjini humiminika kwa wingi na kuijaza manispaa.

Miongoni mwa hao, wapo wanaotegemea usafiri wa umma yaani daladala na wengine wanaosafiri kwa magari yao au vyombo vya maringi mawili.

Yote hayo yakijumuishwa kwa pamoja, kulinganisha na ufinyu wa miundombinu yetu ya barabara, husababisha msongamano mkubwa unaowachelewesha watu kuwahi katika shughuli zao za kujitafutia riziki au mishughuliko mingine ya kila siku.

Adha inakuwa kubwa zaidi pale kunapokuwa na meli au boti zinazowasili katika bandari ya Zanzibar kutoka kisiwani Pemba na Dar es Salaam na pia katika barabara ya Darajani kuelekea soko kuu.