NA ABOUD MAHMOUD, ALLY HASSAN (DOMECO)
SERIKALI ya Zanzibar, imefanikiwa kuongeza thamani ya usafirishaji wa bidhaa za nje ya nchi kwani imeongezeka kutoka kwenye shilingi bilioni 48.6 hadi 65.7 kwa mwaka 2019/2020 sawa na asilimia 35.1.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Jamal Kassim Ali, aliyasema hayo katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani wakati alipokua akiwasilisha mwelekeo wa hali ya uchumi kwa mwaka 2021 na mpango wa maendeleo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Alisema ongezeko hilo limetokana na usafirishaji wa zao la Karafuu kutoka tani 1,744.90 zenye thamani ya bilioni 19.8 kwa mwaka 2019, hadi tani 3,506.8 zenye thamani ya shilingi bilioni 38.37 kwa mwaka 2020.
Pia alisema kuongezeka kwa usafirishaji wa zao la Mwani kutoka tani 11,203.70 zenye thamani ya shilingi bilioni 10.3 kwa mwaka 2019 na kufikia tani 11,382.6 zenye thamani ya shilingi bilioni 11.7 kwa mwaka 2020.
Waziri Jamal alieleza kwamba uingizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi umeongezeka kufikia bilioni 847.4 kwa mwaka 2020 ikilinganishwa na thamani ya shilingi bilioni 755.3 kwa mwaka 2019 sawa na ongezeko la asilimia 12.2.
Sambamba na hayo Waziri Jamal alifahamisha kuwa katika sekta ya kilimo inajumuisha sekta ndogo ndogo za mazao, uvuvi, mifugo na misitu.
Aidha, alisema katika mwaka 2020 ukuaji wa sekta hiyo katika pato la taifa umefikia wastani wa asilimia 3.3 kutoka ukuaji wa wastani asilimia 2.6 kwa mwaka 2019.
Alisema katika ukuaji wa sekta hiyo ya kilimo umetokana na kuongezeka kwa uzalishaji katika sekta ndogo ya mazao kutoka wastani wa asilimia 5.8 kwa mwaka 2019 na kufikia wastani wa asilimia 1.3 kwa mwaka 2020.