NA KHAMISUU ABDALLAH

VIJANA watatu waliodaiwa kufanya kitendo cha wizi katika maeneo ya Mazizini, wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.

Washitakiwa hao ni Zafar Abdalla Zafar (19) mkaazi wa Kwamchina Mwanzo, Exben Hristandus (20) mkaazi wa Chukwani na Mudrik Abass Khamis (20) mkaazi wa Mbweni wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Wote kwa pamoja, walifikishwa katika mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe mbele ya Hakimu Mohammed Ali Haji na kusomewa shitaka linalowakabili na Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya (DPP), Suleiman Yussuf.

Hati ya mashitaka ilidai kuwa, washitakiwa hao wote kwa pamoja walipatikana na kosa la wizi, kinyume na kifungu cha 251 (1) (2) (a) na kifungu cha 258 vya sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Ilidaiwa kuwa, wote kwa pamoja bila ya kuwa na dai la haki na nia ya kujimilikisha, waliiba Vespa moja yenye rangi nyekundu ikiwa na namba za usajili Z 770 DT mali ya Ramadhan Mrisho Rupia, ikiwa na thamani ya shilingi 2,700,000 kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Tukio hilo walidaiwa kulitenda Novemba 25 mwaka 2018 majira ya saa 9:40 jioni huko, Mazizini wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Washitakiwa hao waliposomewa shitaka hilo walilikataa na kuiomba mahakama iwapatie dhamana, huku upande wa mashitaka ukidai kuwa upelelezi wa shauri hilo tayari umeshakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuwasilisha mashahidi.

Hakimu Mohammed, alikubaliana na ombi la upande wa mashitaka na kuiahirisha kesi hiyo hadi Juni 23 mwaka huu na kuamuru upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.

Mahakama, pia iliwataka washitakiwa hao kila mmoja kujidhamini mwenyewe kwa fedha taslimu shilingi 200,000 na kuwasilisha wadhamini wawili ambao kila mmoja atamdhamini kwa kima hicho hicho cha fedha za maandishi, pamoja na kuwasilisha kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi na barua ya Sheha.

Mshitakiwa Mudrik alitimiza masharti hayo na kuachiwa hadi tarehe nyengine aliyopangiwa mahakamani hapo, huku wawili wakishindwa masharti hayo na kupelekwa rumande hadi tarehe nyengine waliyopangiwa mahakamani hapo.