Wengi walalamikia vyombo vya sheria

NA HUSNA MOHAMMED

LICHA ya Zanzibar kuwa na sheria ya Ushahidi Namba. 9 ya mwaka 2016 ambayo imenyima dhamana kwa kesi za udhalilishaji wa kijinsia hasa ubakaji na ulawiti lakini bado baadhi ya watuhumiwa wa kesi hizo hupewa dhamana.

Hali hiyo imepelekea kuongezeka kwa vitendo hivyo huku watoto na wanawake ndio waathirika wakubwa.

Ofisi ya mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar ilisema matukio ya udhalilishaji wa kijnsia yaliokusanywa na taasisi mbalimbali, ikiwemo Jeshi la Polisi, kwa mwaka 2020 ni 1,363.

DHAMANA KWA WASHTAKIWA

Kitendo cha kupewa dhamana kwa baadhi ya washtakiwa wa kesi hizo kimeibua mjadala mkubwa kwa wanaharakati wa kutetea haki za wanawake na watoto pamoja na wahanga wa matukio hayo.

Baadhi ya Wazazi wa watoto waliofanyiwa vitendo vya udhalilishaji wamelalamikia uwepo wa dhamana kwa watuhumiwa wa vitendo hivyo hali inayotowa mwanya kwa wafanyaji wa vitendo hivyo kuendeleza matukio hayo.

Wahanga wa matukio hayo walisema kinachoumiza zaidi kumuona mshtakiwa au mtuhumiwa wa kesi hizo yupo nje kwa dhamana wakati sheria imenyima dhamana kwa watu hao.

WAATHIRIKA WA MATUKIO YA UDHALILISHAJI WAZUNGUMZA

Ali Khamis (sio jina lake halisi) ni miongoni mwa wazazi walielawitiwa na kubakwa mtoto wake wa kike (15) jina tunalihifadhi, alisema anashangaa kumuona mhalifu aliyemharibia mtoto wake yupo mtaani anadunda wakati alishaikabidhi kesi hiyo katika vyombo vya sheria.

Alisema watuhumiwa hao wa kesi hizo wanapokua mitaani huleta vitisho kwa wahanga na familia za wahanga wa vitendo hivyo.

“Mtuhumiwa aliyeniharibia mtoto wangu kwa kumbaka na kumlawiti leo hii yupo mtaani licha ya kumkabidhi katika vyombo vya sheria na hivi sasa amekua akinipa vitisho”, alisema.

Alisema sheria imeshaeleza kuwa kesi hizo hazina dhamana inakuaje watuhumiwa hao wanapewa dhamana.

Fatma Ali (sio jina sahihi) ni mama wa mtoto aliefanyiwa udhalilisha alisema ni vyema sheria ikafuatwa watuhumiwa wa kesi za udhalilishaji wasipatiwe dhamana.

Alisema kitendo cha watuhumiwa hao kupewa dhamana kinawaathiri sana kwa sababu watuhumiwa hao huwa ni watu wa karibu katika familia.

“Wanapopewa dhamana watu hawa, huwa hatuna amani hata kidogo kwa sababu hufika kututishia maisha yetu na wengine hudiriki kutumia njia za ushirikina kwa kutufanyia mambo sio mazuri”, alisema.

Mariyam Khamis Issa, mlezi wa mtoto aliebakwa, ameziomba Mahakama kuharakisha upatikanaji wa hukumu kwa kesi za udhalilishaji ili kuondoa mwanya wa kufanyika vitendo vya rushwa katika vyombo hivyo vya sheria.

Alisema bado kuna mlolongo mrefu wakati wa ufuatiliaji wa kesi hizo hali inayosababisha   uwepo wa rushwa.

Alisema amekuwa akifuatilia kesi zao kwa muda mrefu bila ya kutolewa hukumu na hatimae watuhumiwa kuachiwa huru jambo linalosababisha kuwa na dhana ya kufanyika vitendo vya rushwa ndani ya Mahakama.

Makame Omar ambae watoto wake wawili wamedhalilishwa na Baba wa kambo, alisema baadhi ya watuhumiwa wanapopewa dhamana wanakuwa na kejeli na dharau mbele ya walioathirika na vitendo hivyo.

Alisema ili kupunguza machungu ya madhara yaliyompata mhanga ni vyema mahakama kutotoa dhamana kwa watuhumiwa wa vitendo vya udhalilishaji.

WANAHARAKATI NAO WAZUNGUMZA

Meneja mipango kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Tamwa Zanzibar, Ali Abdallah,amewataka watendaji wanaoshughulikia kesi za udhalilishaji kutokua na muhali katika usimamizi wa sheria.

“Sheria ipo ya kuwa washtakiwa wa kesi hizi kutopewa dhamana sasa inakuaje wanapewa dhama jambo hilo linarejesha nyuma juhudi za wananchi na wanaharakati wa kupinga vitendo vya udhalilishaji”alisema.

Hakimu dhamana wa Mkoa wa Kusini Unguja, Kahmis Ali Simai, alisema katika sheria ya Mahakama haijafuta kifungu cha Jaji mkuu kutoa dhamana katika mahakama kuu hivyo baadhi ya watuhumiwa wanapatiwa dhamana kutokana na sababu maalum.

Alisema kuwa baadhi ya watuhumiwa hulazimika kupewa dhamana kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo za kiafya.

Alifahamisha kuwa baadhi ya washtakiwa wa kesi hizo huwa na matitizo ya kiafya ikiwemo ugonjwa wa kisukari na virusi vya Ukimwi.

Hakimu huyo alisema watu hao huwa wanatumia dozi maalum za dawa na vyakula maalum hivyo kuendelea kuwaweka mahabusu ni kuwazidishia maradhi.

“Kwa mfano kuna mtuhumiwa alikua anakabiliwa na mtihani wa kidato cha sita, sasa usipompa dhamana unaweza kumkosesha haki zake zengine za msingi”, alisema.

Alisema kuwa sio kila mshtakiwa wa kesi hizo huwa na hatia hivyo unapomkosesha kufanya mtihani wake wa shule endapo Mahakama ikimuona hana hatia itakua ushamkosesha elimu.

Alisema kinachofanywa na Mahakam kuu kutoa dhamana huwa wanafuata sheria ambazo zimeelekeza taratibu, hivyo ikiwa watu hawajaridhika na suala la dhamana wanapaswa kukata rufaa.

WANASHERIA

Nae Afisa mipango kituo cha huduma za sheria Zanzibar, Thabit Abdalah Juma, aliwataka wananchi kutambua kuwa utolewaji wa hukumu katika kesi za udhalilishaji  sio jambo rahisi kwani kupatikana mfanyaji wa kitendo hivyo ndio kinachochukuwa muda mrefu ili kuepusha hatia zisizostahiki.

Hivi karibuni Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi alisema hajaridhishwa na utendaji wa jeshi la Polisi katika kushughulikia kesi za udhalilishaji wa kijinsia.

Alisema yapo malalamiko kutoka kwa jamii kwamba jeshi la Polisi limekuwa likifanya upatanishi wa suluhu wa kesi hizo katika vituo vya Polisi na kuzimaliza kienyeji.

Akizungumza na wananchi pamoja na wanachama wa chama cha Mapinduzi wa Mkoa wa Mjini Magharibi hapo makao makuu ya Chama Mkoa Amani mjini Unguja, hivi karibuni alisema wanachokifanya polisi sio kazi yao kwa mujibu wa sheria  ambapo wanatakiwa kuhakikisha wanatayarisha kesi kwa kufanya upelelezi na kuzipeleka mbele kwa hatua nyengine na sio suluhu.

”Nilikutana na viongozi wa jeshi la Polisi,mkurugenzi wa mashtaka pamoja na mahakama na kuwataka wakutane na kuweka utaratibu mzuri utakaohakikisha kesi hizo zinasikilizwa haraka ili jamii iondokane na malalamiko”, alisema.

Dk,Mwinyi aliwapongeza wajumbe wa baraza la wawakilishi kwa kufanya marekebisho mazuri katika sheria za udhalilishaji ambapo mtuhumiwa wa makosa hayo asipewe dhamana.

”Nimemtaka jaji mkuu sheria itekelezwa wanaofanya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwanza wanyimwe dhamana huku shauri lao likiendelea’, ‘alisema.

Jumla ya watu 571 wamebakwa  wakiwa miongoni mwa waathirika wa matukio ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia mwaka 2020.

UKUBWA WA TATIZO

Kwa mujibu wa Kitengo cha Makosa ya Jinai, Madai na Jinsia Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, ambapo inaonesha takwimu za ukatili na udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto.

Miongoni mwa waliobakwa walikuwa wanawake 64 na wasichana 507, waliolawitiwa ni 102, kiingiliwa kinyume na maumbile 46 ambao mwanamke ni mmoja na wasichana 45.

Hata hivyo, mlinganisho wa mwaka 2019 na 2020, umepungua kutoka matukio ya kubaka 651 hadi 571, kulawiti matukio 157 hadi 102.

Kitengo hicho, kilisema jumla ya matukio 1,363 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa mwaka 2020 ambapo wanawake na watoto wamekuwa waathirika wakuu.

Aidha waathirika 217 walikuwa wanawake sawa na asilimia 15.9 na watoto 1,146 sawa na asilimia 84.1, miongoni mwao wasichana 899 (asilimia 78.4) na wavulana walikuwa 247(asilimia 21.6).

Wilaya zinazoongoza ni Mjini ndiyo iliyoshika nafasi ya kwanza ikiwa na matukio 297, ikifuatiwa na Magharibi ‘B’, matukio 273 na Micheweni ikiwa na idadi ndogo ya matukio 41.

Hata hivyo, idadi ya matukio  kwa mwaka uliopita  imepungua kidogo kwa asilimia 0.4 kutoka matukio  1,369  mwaka 2019 hadi 1,363 maka 2020.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa watoto wenye umri wa miaka 15-17 wameripotiwa kuwa na idadi kubwa ya matukio 681 sawa na asilimia 59.4 ya matukio yote ya watoto ni zaidi ya robo mbili ukilinganisha miaka mengine ya watoto.

Aidha matukio mengi yameonesha kutokea majumbani yakiwa ni 1,270 sawa na asilimia 93.2, ikifuatiwa na sehemu neyngine ikiwemo kazini, skuli na madrasa.

Nae Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Wanawake na Watoto, Nasima Haji Chum, alisema, serikali inaumizwa na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na inaendelea kupanga mipango madhubuti ya kutokomeza vitendo hivyo.

Alisema vitendo vya udhalilishaji vinaendelea kuzungumziwa kwa upana katika taasisi mbali mbali nchini, hivyo, lengo na azma  iliyokusudiwa na serikali ni kuvikomesha vitendo hivyo miongoni mwa wanajamii.

Mkurugenzi huyo, aliwataka wazazi kuwa karibu katika kusimamia malezi ya watoto katika maisha yao wanayoishi kila siku ili kuelewa iwapo kutatokea kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji.

Aidha, alisema, wizara husika itaendelea kushirikiana na wananchi katika vita vya kupambana na vitendo  vyote vya udhalilishaji wa kijinsia kwa ajili ya ustawi wa jamii.

Ili kushinda vitendo hivyo, jamii, wanaharakati na wadau hawanabudi kushirikiana na serikali ili kuwatia hatiani na kukubali kutoa ushahidi makahakamani kwa wanaohusika.