NA HAROUB HUSSEIN

MAMLAKA ya Vyuo vya Amali Zanzibar (VTA) imeeleza mpango wa kujenga vyuo vipya vya amali katika Wilaya zote Unguja na Pemba, umelenga kutoa fursa kwa vijana kusomea fani zinazopatikana katika Wilaya husika.

Hayo yalielezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo, Dk. Bakari Ali Silima, wakati wa mahafali ya nane ya Chuo cha Mafunzo ya Amali Mkokotoni, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema kuwa katika kutatua changamoto ya ajira kwa vijana na kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020/2025 mamlaka hiyo ina mpango wa kuanza ujenzi wa vyuo vyake katika Wilaya zote na kwa kuanzia itaanza na ujenzi wake katika Chuo cha Wilaya ya Kaskazini ‘B’.

Dk. Bakari alisema wameamua kuanza na wilaya hiyo ili kuziwahi fursa zitazopatikana katika uchumi wa buluu kwa kuwahi soko la ajira litakalokuwepo wakati wa ujenzi wa bandari ya mafuta ya Mangapwani.

Aidha alisema katika kufikia lengo hilo wanaiomba Serikali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja kuwapatia eneo litalokua katika Wilaya ya Kaskazini ‘B’ ili kuanza kwa ujenzi huo.

Alisema katika chuo hicho fani zitakazopewa kipaumbele ni zile zenye kwenda sambamba na harakati za ujenzi wa bandari ya mkokotoni, ili vijana waweze kutumia fursa za ajira zitakazopatikana katika ujenzi huo.

Aidha alisema katika mahafali hayo jumla ya wahitimu 138 wamemaliza masomo yao katika fani tofauti chuoni hapo, wakiwemo wanaume 88 na wanawake 50.

Akihutubia katika mahafali hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud, Mkuu wa wilaya ya Kaskazini ‘A’, Sadifa Juma Khamis, alisema kuanzishwa kwa vyuo vya amali kumepunguza tatizo la ajira kwa vijana kutokana na wahitimu wengi kujiajiri katika fani wanazosomea.