NA LAYLAT KHALFAN

KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar, (ZATUC), Khamis Mwinyi Mohamed, amewasisitiza waajiiri kufuata sheria na kanuni za kazi ili kupunguza migogoro  isiyokuwa na tija katika sehemu za kazi.

Aliyasema hayo katika hoteli ya Beach Resort, Mazizini wakati wa mkutano wa kuwajengea uwezo viongozi wanawake wa vyama vya wafanyakazi kwa lengo la kujua haki zao.

Alisema sheria zimewekwa kwa ajili ya kuleta maslahi kwa wafanyakazi na waajiri na kuondosha changamoto nyingi zinazojitokeza kazini kwa lengo la kupata ustawi kwa taifa.

Alisema tatizo la Zanzibar linatunga sheria nzuri lakini wakati wa utekelezaji vyombo vinavyotumia sheria hiyo haitekelezaji ipasavyo na kusababisha vita kwa kila taasisi.

“Kutokana na hili tunaiomba serikali kuhakikisha kuwa sheria zote zinazotumiwa na baraza la wawakilishi zinasimamiwa ipasavyo na zinafatwa ili kila mfanyakazi apate stahiki zake zinazokubalika kisheria,” alisema Mwinyi.

Sambamba na hilo aliwataka wafanyakazi kujiunga na vyama hivyo kwa kuvitumia na kuviunga mkono ili kupata nguvu ya kutetea haki zao pale inapotokezea matatizo.

Aidha, Katibu huyo alisema mfanyakazi mmoja mmoja kamwe hawezi kutetea haki yake, hivyo ni vyem kushirikiana katika kufanikisha suala hilo kwa kupeleka malalamiko yao katika maeneo husika ili kusimamiwa katika vyombo husika na kupatiwa ufumbuzi wa haki.

Akifungua mafunzo hayo ya siku tatu, Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho hilo, Bimwanamkuu Gharib Mgeni, alisema wafanyakazi wanawake katika sehemu za kazi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi kwa kutokana na kukosa uelewa juu ya umuhimu wa kujiunga na vyama hivyo.

Alisema jumuiya hiyo haipenda kuona migongano ndani ya vyama vya wafanyakazi kwani ni miongoni mwa sababiu zinazotajwa kuwa sababu ya kusambaratika kwa baadhi ya vyama ambayo ndio mkombozi mkubwa kwa wafanyakazi wake.

Sambamba na hayo aliwaomba wanachama hao kuwa mabalozi wazuri wa kupeleka mfunzo hayo huko wanako kwenda kwa kuhakikisha yanafanyiwa kazi ili kufikia malengo yliyokusudiwa.

Washiriki wa mafunzo hayo, walipongeza juhudi za ZATUC kwa kupatiwa mfunzo hayo kwani walikuwa hawajui namna ya kujitetea wanapokuwa kazini pale wanapofikwa na matatizo.