NA ABOUD MAHMOUD

WABUNGE kutoka nchini Kenya wameeleza kuridhishwa na mwenendo wa maisha ya wananchi wa Zanzibar na kwamba wamejifunza mambo mengi yenye faida kwa watu wao.

Hayo yamesemwa na Mbunge wa Kaunti ya Nyandarua, Faith Warimo Ngitau, alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika viwanja vya michezo Mafunzo Kilimani mjini Unguja kufuatia ziara ya wiki moja ya wabunge hao Zanzibar.

Alisema ingawa ziara hiyo ni ya michezo, wamepata fursa ya kutembelea maeneo mbali mbali na kujifunza mambo mengi ukiwemo ustaarabu na maisha ya wananchi wa Zanzibar.

“Kwa kweli tumefarijika sana, ziara yetu hii na tumevutiwa na mambo mbali mbali yakiwemo ya kijamii pamoja na mandhari ya fukwe,” alisema.

Mbunge huyo alifafanua kwamba wakiwa visiwani humu wamejifunza kwamba wananchi wa dini, makabila na kabila tofauti wanaweza kuishi pamoja bila ya kubughudhiana jambo ambalo ni adimu katika maeneo mengine ulimwenguni.

“Tumeshuhudia hapa Zanzibar mtu akitaka kukwambia kitu chochote anatanguliza neno naomba, huu ni ustaarabu wa ajabu na jambo zuri kwetu,” alieleza mbunge huyo.

Aliongeza kwa kusema kuwa; “Nchi mbali mbali nilizowahi kutembelea hakuna mtu anakwamba naomba tupige picha au naomba twende tukale, hili neno limetupa faraja na kuona kwamba nchi hii ni ya kistaarabu lazima tuige hizi tabia,”.

Sambamba na hayo Mbunge huyo alisema pia wamejifunza masuala ya uongozi ikiwemo mashirikiano baina ya Rais wa Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania somo linalopaswa kuigwa na viongozi wengine wa ukanda wa Afrika Mashariki.

“Ingawa Tanzania ni moja lakini ina viongozi wakuu wawili, wamekuwa na mashirikiano mazuri ambayo yanawaletea wananchi wake wote maendeleo katika sekta mbali mbali,” alieleza Faith.

Aidha Faith alisema pia ujio wao umewafunza umuhimu wa uongozi kwa wanawake kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambae ni kiongozi wa kwanza kushika wadhifa huo kwa nchi za Afrika Mashariki.

Wabunge hao waliwasili Unguja Ijumaa iliyopita kwa mwaliko wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ambapo ziara hiyo inatarajiwa kukamilika kesho ambapo mbali ya kushiriki katika michezo mbali mbali, walipata fursa ya kutembelea maeneo ya kihistoria pamoja na kukutana na viongozi wa ngazi mbali mbali wa Zanzibar.