1: PELE

GWIJI na mfalme wa soka kutoka Brazil anayetajwa kama mchezaji bora namba moja kuwahi kutokea duniani.

Hakuna mchezaji aliyewahi kushinda makombe mengi ya dunia kama yeye. Hilo pekee linaweza kumfanya awe mchezaji bora wa wakati wote.

Kashinda makombe manne ya dunia akiwa na Brazil pamoja na mataji saba ya ligi kuu akiwa na klabu yake ya Santos huku akiifungia klau hiyo mabao zaidi ya 600.

Pele pia ameifungia timu yake ya taifa ya Brazil mabao 77 katika michezo 92 tu aliyoichezea, akiwa na rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kufunga katika fainali za kombe la dunia, akifunga mabao mawili dhidi ya Sweden katika michuano ya mwaka 1958.

Usisahau kwamba Pele ni mmoja kati ya wachezaji wanne duniani kufunga katika fainali nne tofauti za kombe la dunia (1958,1962,1966 na 1970).

2: DIEGO MARADONA

Huyu mwamba alikua ana uwezo wa ‘kutembea na kijiji’na kufunga mabao atakayo kwa ubora na burudani. Anafahamika zaidi kwa goli lake la ‘mkono wa Mungu’ alilowachapa England katika michuano ya kombe la dunia la mwaka 1986.

Ameweka alama akiwa na klabu za Argentinos Juniours, Boca Juniours, Barcelona, Napoli, Sevilla, Newell’s Old Boys na timu ya taifa ya Argentina akifunga mabao zaidi ya 300 katika maisha yake ya soka.

3: LIONEL MESSI

Yeye pamoja na Christiano Ronaldo wanatajwa kama wachezaji bora wa kizazi cha sasa, anatumikia Argentina na klabu yake ya Barcelona. Ni mchezaji pekee kuwahi kutokea kuzoa tuzo sita za mchezaji bora wa soka duniani ‘Ballon d’Or.

Ingawa hajapata mafanikio sana kwenye timu yake ya taifa kama alivyopata akiwa na klabu yake ya Barcelona, kipaji cha Messi na uwezo binafsi wa kucheza na mpira, kutoa pasi murua za magoli pamoja na kufunga kunamfanya kuwa miongoni mwa wachezaji bora wa muda wote.

4: CHRISTIANO RONALDO

Tofauti yake na Messi, ni kwamba Ronaldo ametwaa taji akiwa na timu ya taifa ya Ureno, akitwaa kombe la Euro 2016, Messi mpaka leo anatafuta kombe akiwa na Argentina, kitu ambacho kinakosekana kwenye kabati lake la makombe aliyowahi kutwaa kwenye maisha yake ya soka.

Ronaldo ametwaa tuzo tano za mchezaji bora wa dunia ‘Ballon d’Or, katika miaka yake karibu 16 ya kucheza soka. Licha ya umri kumtupa, Ronaldo anaendelea kuitumikia timu yake ya taifa akiendelea pia kutupia mabao akiwa na klabu yake ya Juventus ya Italia.

5: YOHAN CRUYFF

Huyu ndiye aliyeleta aina ya soka inayofahamika sasa kama ‘total football’, akifanya maajabu na klabu yake ya Ajax ya Uholanzi. Alipojiunga na Barcelona, ilikuwa na ukame wa vikombe, akabadilisha upepo uliodumu kwa miaka 14.

Kuna wakati Rais wa Barcolona, Joan Laporta aliwahi kusema, Cruyff alikuja duniani kuleta sanaa na burudani kwenye soka na sio kucheza tu. Amekuwa mchezaji bora wa dunia mara tatu, akidumu kwa zaidi ya miaka 20 kwenye soka.

6: RONALDO DE LIMA

Ukitakata kujua ukali wa Mbrazil huyu, rejea kombe la dunia la mwaka 1998 na 2002. Mwaka 1998 alifunga mabao manne na kutengeneza matatu, lakini kombe la dunia la mwaka 2002, alionyesha dunia kwamba anastahili kuheshimiwa kwa kupachika mabao manane na kutwaa kiatu cha dhahabu akiisaidia Brazil kutwaa taji lao la tano la kombe la dunia.

Amewahi kuwa mchezaji bora wa soka duniani mara mbili mwaka 1997 na 2002, akipata mafanikio kwenye vilabu vya Barcelona, Inter Milan, Real Madrid na AC Milan.

7: FRANZ BECKENBAUER

Mchezaji bora mara mbili wa Ulaya wa mwaka 1972 na 1976, akiwa mchezaji pekee duniani kushinda kombe la dunia kama mchezaji na kama kocha akiwa na Ujerumani.

Amezichezea klabu kadhaa ikiwemo Bayern Munich alikotwaa mataji manne ya Bundersliga na manne ya Ulaya, likiwemo Klabu bingwa mwaka 1972.

8: ZINEDINE ZIDANE

Ni mmoja kati ya wachezaji wachache kuwahi kushinda kombe la dunia, kombe la mabingwa Ulaya na kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia.

Alikuwa mchezaji bora wa dunia mwaka 1998, amewahi pia kuwa mchezaji bora wa mashindano ya UEFA Euro 2000 na akaisaidia Ufaransa kutwaa kombe hilo na akawa pia mchezaji bora wa mashindano ya kombe la dunia ya mwaka 2006.

Ameichezea Ufaransa michezo 108 akifumania nyavu mara 31, lakini jina lake lilikuwa juu zaidi wakati Ufaransa inatwaa kombe la dunia mwaka 1998 akifunga mabao mawili kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Brazil.

9: FARENC PUSKAS

Anatajwa kama mshambuliaji wa kuogopwa kuwahi kutokea, akiliona lango kufunga kwake ni kama kunywa chai ya jioni. Katika maisha yake ya soka la kulipwa amefunga jumla ya mabao 808 na kuwa mfungaji namba tatu wa muda wote duniani.

Ameifungia timu yake ya taifa magoli 84 katika michezo 85 ya kimataifa ailiyochezea. Ametwaa mataji 10 ya ligi kuu, matano ya Hispania na matano ya ligi kuu ya Hungary, akifunga mabao 514 katika mechi 529.

10: ALFREDO D STEFANO

Ana asili ya Argentina, Lakini amepata umaarufu akiwa na Hispania. Amecheza timu tatu za taifa: Alianza Argentina mwaka 1947 akifunga mabao 6 katika michezo 6, akaichezea Colombia michezo miwili mwaka 1949 kabla ya kujikita na Hispania kuanzia mwaka 1957 mpaka 1962 akiifungia mabao 23 katika michezo 31. Anatajwa kama mchezaji aliyekamilika zaidi, akiwa na nguvu, uwezo, kipaji cha kunyumbulika na akili ya hali ya juu ya mpira.

Mwaka 1957 na mwaka 1959 alicheza soka la hali ya Juu Ulaya, kiasi cha kutwaa karibu kila tuzo za wakati huo. Kwa sasa anashika nafasi ya sita katika wachezaji wanaongoza kwa kufunga mabao mengi kwenye ligi kuu ya Hispania, wakati huo akizichezea timu mbalimbali za ligi hiyo ikiwemo Real Madrid na Valencia.