JOHANNESBURG, Afrika Kusini
NYOTA wa timu ya taifa ya Brazil na PSG, Neymar da Silva Jr., amesema, kuna tofauti kubwa kati ya wachezaji wa timu ya taifa lake, na wale wanaotoka kwenye mataifa ya Afrika, pindi wanapokua kwenye majukumu ya kimataifa.

Neymar ambaye kwa sasa yupo nchini kwao kwa ajili ya kushiriki kushiriki michuano ya fainali ya Kombe la Mataifa ya Kusini mwa Amerika (Copa Amerika), alieleza hayo kufuatia utofauti unaonekana kwenye kikosi cha mabingwa hao mara tano wa dunia, na mataifa mengine duniani, hususan ya Afrika.

Alisema wachezaji wengi wa Afrika wana vipaji vya hali ya juu, lakini, hawajitumi wakiwa katika timu zao za taifa, na matokeo yake hujikuta wanashindwa kuzisaidia na kuwekeza nguvu nyingi kwenye klabu zao huko Ulaya ama kwengineko duniani.

Pia, Neymar, alieleza kuwa wachezaji Waafrika hawana mwamko wa kucheza katika timu zao za taifa kama ilivyokuwa wachezaji wa Amerika ya Kusini

“Wachezaji wengi wa Afrika wana vipaji vya hali ya juu, lakini, hawajitumi wakiwa katika timu zao za taifa, hiyo ndiyo tofauti yao na sisi Brazil ambayo kwa sasa tuna makombe matano ya Kombe la Dunia”.

“Nyota wa Waafrika hawana mwamko wa kucheza katika timu zao za taifa, lakini, wanacheza katika klabu bora za Ulaya na wanaonyesha uwezo wa juu”.

Wachezaji nyota kadhaa wa Afrika wamekuwa kwenye malumbano na mashabiki wa mataifa yao, kufuatia kuonesha viwango duni wanapokua kwenye jukumu la kuzutumikia timu zao za taifa, wakilinganishwa na wanapokuwa ndani ya uwanja kwenye klabu zao.(AFP).