NA TATU MAKAME

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Dk. Khalid Salum Mohammed, ameyataka mashirika ya maendeleo na taasisi za uwekezaji kuendelea kuisaidia Zanzibar kuendeleza uchumi wa buluu ili kufikia malengo ya kukuza uchumi.

Dk. Khalid alisema hayo wakati akifunga kongamano la siku moja la uchumi wa buluu kwa maendeleo ya kijamii,Kiuchumi na uhifadhi wa Mazingira lililofanyika katika hoteli ya Verde Mtoni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Kongamano hilo lililoandaliwa na taasisi ya uongozi, Shirika la Maendeleo la Umoja wa  Mataifa (UNDP) na Shirika  la Umoja wa Mataifa la Uhifadhi wa Mazingira la (UNEP), .

Alisema Serikali ya awamu ya nane chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, imedhamiria kuimarisha uchumi wa buluu  kupitia sekta ya uvuvi  wa bahari kuu hivyo ipo haja kwa mashirika na taasisi hizo kuendelea kuunga mkono sekta hiyo.

“Serikali ya awamu ya nane jinsi ilivyojikita katika kuendeleza uchumi wa buluu tunapaswa sote tuunge mkono juhudi hizi za Mheshimiwa Rais Dk. Mwinyi kwani yeye ni chachu ya uchumi,” alisema.

Alisema kwa kuhakikisha azma hiyo inafikiwa, Dk. Mwinyi, aliunda Wizara maalum ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi katika masuala mazima ya kuimarisha miundombinu itakayosaidia kuunga mkono ajenda hiyo ya uchumi wa buluu kwa maendeleo endelevu katika nchi.

“Na mfano wa hayo ni bandari itakayojengwa Mangapwani na bandari ya mpigaduri hizo ni ishara za kuwa Rais amedhamiria kikwelikweli katika kuendeleza sekta hii,” alisema.

Aidha Dk. Khalid alisema umefika wakati wa kufanya kwa vitendo katika kuendeleza uchumi wa buluu ili nchi iweze kupiga hatua ya maendeleo.

Alisema kwamba alisema serikali ya Mapinduzi Zanzibar inahitaji wawekezaji watakaoendeleza uchumi wa buluu kwa kuendelea kuwahamasisha kuja kuekeza kwenye sekta hiyo hapa nchini.

Aliwataka waandishi wa habari kuendelea kuielimisha jamii kuhusu dhana ya uchumi wa buluu ili kila mmoja atimize majukumu yake kwenye sekta hiyo.

Kwa upande mwengine, Dk. Khalid, aliwataka Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuifikisha ajenda hiyo ya uchumi wa buluu majimboni mwao ili wananchi wajue kila kinachofanyika katika kuendeleza sekta hiyo ya uvuvi hapa Zanzibar.

“Suala hili ni mtambuka kunahitaji mashirikiano kwa sekta zote iwe wawekezaji kwa kufanya biashara ya kununua na kuuza kwani raslimali zipo za kutosha na kuendeleza uchumi wa buluu,” alisema.

Mapema Mwakilishi wa Shirika la Mipango ya maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Chritine Musisi, alisema wako tayari kuisaidia Zanzibar katika kukuza na kuendeleza uchumi wa buluu ili kuona uchumi wa Zanzibar unakua.

Hata hivyo aliwataka washirika wengine wa maendeleo kuendelea kuiunga mkono Zanzibar kupitia uchumi huo na kuona Zanzibar inafikia kwenye mataifa mengine duniani yaliyoanzisha uchumi huo.

Wakichangia mada ya uchumi wa buluu washirika wa kongamano hilo waliwataka wazalishaji wa mazao ya baharini kuongeza ubora kwenye vyakula ili kupata soko katika nchi nyengine.

Hata hivyo washiriki hao waliitaka serikali kuendelea kufanya utafiti za mwani wenye thamani na wakulima waweze kulima zao hilo kwenye kina kikubwa cha maji na kuongeza pato lao.