NA ABOUD MAHMOUD

WADAU wa soka kisiwani Unguja wamemshauri Rais mpya wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) Abdulatif Yassin Ali, kuhakikisha anaweka misingi madhubuti itakayoleta maendeleo ya mchezo huo.

Waliyasema hayo wakati walipokutana na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu uliofanyika Jumapili iliyopita katika ukumbi wa Makao makuu ya chuo cha mafunzo Kilimani mjini Unguja.

Walisema kutokana na matatizo mbali mbali yanayolikabili shirikisho hili ni vyema kiongozi huyo kuhakikisha anaondosha tofauti zilizokuepo pamoja na kuleta maendeleo ambayo wadau wa soka wanayahitaji.

“Tayari ZFF ishapatikana Rais mpya, tena kijana mwenyewe na afahamu kwamba nafasi aliyopewa ni kubwa na Zanzibar nzima inamtizama yeye kama inavyomtizama Dk. Mwinyi, ushauri wangu awe makini na ajue kwamba sisi wadau wa soka tunataka mabadiliko sio malumbano,” alisema Omar Makubela.

Omar alisema ni wajibu wa kiongozi huyo kuhakikisha kwanza anaondosha makundi yaliyomo ndani ya uongozi wa ZFF yaliyochafua hadhi ya soka la visiwani humu.

Nae Suwedi Fadhil alimshauri Rais huyo kuhakikisha anavisaidia vilabu kuanzia ligi za chini mpaka ligi kuu ili viweze kucheza soka bila matatizo.

“Namuomba ahakikishe anavisaidia vilabu vyetu kwani vina changamoto mbali mbali hususan hivi vya chini ajitahidi kututafutia wadhamini ili tufikie mbali mpaka ligi kuu,” alisema.