HAFSA GOLO NA KHAIRAT SULEIMAN (MCC)
WAJUMBE wa Baraza la wawakilishi wameishauri Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kufanya utafiti, kufuata sheria na kusimamia utekelezaji wa mipango ya nchi ili kufikia dhana ya maendeleo endelevu.
Ushauri huo umetolewa na mwakilishi wa jimbo la Pangawe, Ali Suleiman Mrembo, wakati akichangia hutuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya uchumi wa buluu na uvuvi kwa mwaka wa fedha 2021 /2022 katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani.
Alisema iwapo viongozi na watendaji watasimamia ipasavyo mambo hayo, upo uwezekano wa kufikia malengo yaliyokusudiwa na serikali kwa wakati muwafaka katika sekta mbali mbali ikiwemo ya mafuta na gesi asilia na uvuvi badala ya kufuata mitazamo ya nchi nyengine.
Alisema Mamlaka ya udhibiti na utafutaji wa mafuta na gesi asilia (ZPRA) inapaswa kuwasilisha kanuni zote zilizoelezwa katika kitabu cha bajeti kwa kamati ndogo ya baraza hilo hususan kanuni ya uhifadhi wa taarifa za utafutaji wa mafuta na gesi asilia.
Akizungumzia Kampuni ya maendeleo ya mafuta na gesi asilia (ZPDC), Suleiman alisema kampuni hiyo haijaanza kufanya kazi vizuri kutokana na kampuni hiyo kutopewa nguvu.
“Ili kampuni hiyo iweze kuwa na nguvu lazima ipewe nyenzo zitakazoiwezesha kujitegemea jambo ambalo halijafanyika,” alisema.
Alifahamisha kwamba hatua hiyo iende sambamba na kuwajengea uwezo watendaji wa ndani ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Nae Mwakilishi wa jimbo la Mkwajuni, Sulubu Kidongo Amour, aliishauri wizara hiyo kuhakikisha inasimamia ipasavyo sekta ya uvuvi ikiwa ni pamoja na matumizi mazuri ya kisheria na taratibu zilizopo nchini.
“Nakuomba Waziri ukaisimamie sekta ya uvuvi na watendaji wako wakasimamie majukumu yao kwa mujibu wa miongozo na taratibu za kisheria,” alisema.
Alisema fedha zilizotengwa ndani ya bajeti hiyo lazima zifuate utaratibu zikiwemo za ununuzi wa vitenda kazi vya uvuvikwa lengo la kuwakomboa wanyonge kama ilivyo dhamira ya serikali.
Kuhusu zao la mwani, Sulubua alisema ni vyema watendaji wakafanye utafiti juu ya upandaji wa zao hilo pamoja na kuwaelimisha wakulima ili waweze kupata mafanikio.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa jimbo la Chwaka, Issa Haji Ussi ‘Gavu’, alisema ni vyema wataalamu wanapopanga mipango kuhusiana na masuala ya uvuvi kuwatumiwa wavuvi ili waweze kubaini maswla muhimu na kuleta mageuzi ya maendeleo katika eneo hilo.
Kuhusu mafuta na gesi alisema, alisema serikali zote mbili zimeandaa njia sahihi za kisheria katika usimamizi wa rasilimali hiyo ili kuondoa mivutano pande mbili hizo katika utekelezaji wake.
Gavu aliongeza kuwa mipango mizuri ya serikali itasaidia kuleta mafanikio iwapo utekelezaji wake utahusisha kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani ili watekeleze majukumu yao ya kazi kwa ufanisi na kuleta tija.
Alisema katika mkataba wa mgawanyo wa mafuta na gesi asilia uliotiwa saini Oktoba 23, 2018 umeweka utaratibu mzuri wa utekelezaji wake kwa miaka 10 iliyowekwa katika vipindi vya miaka 4, 3, 2, 1.
Akizungumzia kuhusu Kamapuni ya Rak Gas alisema kwamba inapaswa kurejesha nusu ya ‘block’ la utafutaji wa mafuta na gesi la Unguja – Pemba ifikapo mwakani.
Alisema kufuatia mipango hiyo ambayo serikali tayari imeshayatekeleza hivyo alimuomba waziri kutoa taarifa juu ya kampuni hiyo hatua zilizofikiwa katika utafutaji wa mafuta na gesi.
Kwa upande wake mwakilishi Azza January Joseph, alisema suala la kupatiwa elimu kwa wavuvi kuwa na bima ya maisha jambo ambalo litasaidia kuipatia fedha serikali lakini pia kuwahakikishia usalama wanapokuwa kazini.
Pamoja na hayo alisema, serikali ingalie kwa karibu wanawake ambao wanajishughulisha na masuala ya uvuvi ikiwemo uuzaji wa samaki ili waweze kunufaika na uchumi wa buluu.
Nae Mwakilishi wa jimbo la Malindi, Mohamed Ahmada Salum, alitilia mkazo suala la mafuta na gesi kwa kuiomba wizara hiyo kuonesha mkakati uliopo katika eneo hilo kwa upande wa Zanzibar hasa ikizingatiwa fedha nyingi zimetumika katika utafiti wa eneo hilo.
Mwakilishi wa jimbo la Ziwani, Suleiman Makame Ali, alishauri serikali wakati wote inapokusudia kufanya uwekezaji wa miradi ya maendeleo, ni vyema kufanya utafiti na tathmini ya mapema ili wananchi wapatiwe stahiki zao badala ya kufanya utafiti baada ya utekelezaji kwani hupoteza uhalisia wake.