NA TUWERA JUMA, MCC

OFISI ya Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii, imesema inakabiliwa na changamoto ya kupokea idadi kubwa ya maombi ya usajili wa vizazi hai vilivyo nje ya wakati.

Mkuu wa kitengo cha huduma za sheria katika ofisi hiyo, Hamid Haji Makame alieleza hayo jana huko ofisini kwake Mazizini alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema kutokana na changamoto hiyo, ofisi hiyo inaendelea na utafiti kubaini kinachosababisha kuongezeka kwa idadi kubwa ya maombi ya usajili wa kizazi hai cha nje ya wakati au kilichochelewa kusajiliwa.

Alisema baada ya kumalizika kwa utafiti huo ambao utaonesha sababu ya kuchelewa kwa usaliji wa vizazi nje ya wakati, ofisi hiyo italazimika kuchukua hatua muafaka za kuondokana na changamoto hiyo.

Alifahamisha kuwa ofisi hiyo ina maombo yanayofikia 5,642 ya usajili wa vizazi hai vilichochelewa, ambapo hata hivyo yanafanyiwa kazi.

“Kati ya maombi hayo, 982 yamegundulika kuwa na kasoro mbalimbali na zaidi ya maombi 300 yamekataliwa kutokana na waombaji husika hawakuzaliwa Zanzibar”, alisema mkuu huyo.

Alisema ofisi inapanga kuwachukulia hatua za kisheria ikiwemo kuwafungulia mashitaka wale waliobainika kutoa taarifa za udanganyifu na kula viapo vya uongo wakati walipoomba usajili wa vizazi hai.

Mkuu huyo alitumia fursa hiyo kuwashauri wananchi wakaazi wa Zanzibar kusajili matukio ya kijamii kwa wakati na baadae wafike ofisi za kila wilaya kwa ajili ya kupata vyeti husika vinavyotokana na usajili huo.

Katika hatua nyengine mkuu huyo alisema ofisi hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kusajili vizazi ndani ya wakati (timely registration), ambapo hali hiyo inatokana na muamko mkubwa na wananchi kufahamu umuhimu wa usajili.

Alitaja baadhi ya matukio yanayosajiliwa na ofisi hiyo ni pamoja na cheti cha kuzaliwa, cha usajili wa ndani ya wakati siku 42 baada ya kuzaliwa na kuomba ndani ya wakati miezi mitatu.

Cheti cha kuzaliwa cha usajili wa ndani ya wakati siku 42 baada ya kuzaliwa na kuomba ndani ya miezi mitatu, usajili mwengine ni cheti cha kifo, fomu ya maombi ya kuzaliwa nje ya wakati, cheti cha kuzaliwa au kifo kilichopotea au kuharibika.