WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imesema jumla ya walimu 1400 wanadai nauli zao  Unguja na Pemba

Waziri wa Wizara hiyo, Simai Mohammed Said alitoa kauli hiyo wakati akijibu suala la nyongeza liloulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Haji Shaaban Waziri katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chuwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Mwakilishi huyo alitaka kujua ni walimu wangapi wanaodai fedha zao za nauli na posho kwa Unguja na Pemba.

Alisema hadi Disemba mwaka 2020 jumla ya walimu kisiwani Pemba  ni 430 wadai jumla ya shilingi milioni 43.

Waziri Simai alisema kutoka mwezi Machi 2018 hadi Januari 2021 walifikia walimu 946 na kufikia zaidi ya shilingi milioni 94.

Kwa walimu wanaodai nauli kuanzia Septemba mwaka 2020 hadi Mei 2021 ni zaidi ya shilingi milioni 100 kwa upande wa kisiwa cha Pemba huku Upande wa Unguja wakiwa ni 970 wanaodai zaidi ya shilingi milioni 300.

Hata hivyo alisema hakuna mwalimu anaedai pesa za likizo huku akibainisha kuwa posho la likizo hulipwa kila baada ya miezi mitatu.

Alisema kutokana na janga la korona sekta mbalimbali zimeyumba kiuchumi hivyo katika bajeti iliyopitishwa wataweza kuitumia ili kuweza kutatua changamoto hiyo ya kulipa madeni ya walimu.

Nae, Mwakilishi wa Jimbo la Wingwi, Kombo Mwinyi Shehe, alisema walimu wengi wanafanya kazi katika maeneo ya mbali wanayoishi sasa kucheleweshewa kupewa nauli zao haionekani kwamba ni Changamoto.

Alisema serikali inapotangaza ajira huwa haiangalii mtu anatokea wapi wala eneo bali inaangalia ubunifu wa kazi kwa muombaji.

Hata hivyo, allibainisha kuwa serikali ina malengo ya kujenga nyumba za walimu katika maeneo mbalimbali ili kutatua changamoto hiyo.

Akijibu suala la msingi liloulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Uzini, Haji Shaaban Waziri, alietaka kujua kwanini walimu hao hawajalipwa fedha zao na muda umeshakuwa mkubwa Waziri Simai, alikiri kuwa ni kweli muda mrefu umepita kwa walimu kutolipwa nauli zao hali ambayo inatokana na kutopatikana OC za kutosha za kulipia walimu hao.

Hivyo aliwaomba walimu wote wanadai malipo ya nauli waendelee kustahamili na mara tu wizara itakapoingiziwa fedha za matumizi ya kawaida OC walimu hao watalipwa fedha zao kwa kufuata taratibu na sheria za serikali zilizokuwepo.

Alisema wizara tayari imeweka utaratibu mzuri ikiwemo kutayarisha vocha za malipo za kila mtumishi ambae anadai nauli kwa ajili ya malipo.