NA MWAJUMA JUMA

ZOEZI la usaili kwa waliochukua fomu za kuwania urais wa Shirikisho la Soka visiwani Zanzibar (ZFF) lilifanyika jana katika ofisi za Shirikisho hilo Amaan mjini Unguja.

Zoezi hilo ambalo lilifanyika kwa amani na usalama liliwashirikisha wagombea wote watano ambao walijitokeza kuchukua fomu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi Fadhil Ramadhan Mberwa alimwambia mwandishi wa habari hizi, kwamba jumla ya wagombea watano walichukua fomu na wote walifanyiwa usaili.

Aliwataja wagombea hao kuwa ni pamoja na Suleiman Mahmoud Jabir, Abdulatif Ali Yasin, Suleiman Ramadhan, Haji Sheha na Abdulkadir Mohammed Abdulkadir ‘Tashi’.

“Zoezi limekwenda vizuri tunashukuru na mara baada ya kumalizika kwa zoezi hilo, tunajiandaa kwa ajili ya pingamizi na kampeni”, alisema.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na kamati hiyo ya uchaguzi  Juni 20 kutakuwa na zoezi la pingamizi litakalokwenda sambamba na kampeni ambazo zitamalizika Juni 26 saa 6:00 usiku na Juni 27 kutafanyika uchaguzi rasmi ambapo wajumbe watapata nafasi ya kumchagua rais.

Uchaguzi huo unafanyika baada ya aliyekuwa rais wa Shirikisho hilo Seif Kombo Pandu kujiuzulu mapema mwaka huu.