RIPOTI mpya iliyotolewa na ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na dawa na uhalifu UNODC, imeeleza kwamba idadi ya watu wanaotumia mihadarati duniani inaongezeka kwa kasi kubwa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika mwaka 2020 duniani kote takriban watu milioni 275 walitumia dawa za kulevya, ikiwa ni ongezeko la asilimia 22 tangu mwaka 2010.
UNODC ilieleza kuwa takwimu hizo ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na ofisi hiyo ambao pia unatoa mtazamo wa jumla wa soko la mihadarati duniani pamoja na athari zake kwa afya za watu na maisha yao katika mtazamo wa janga la corona au COVID-19.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo matumizi ya bangi yameongezeka mara nne katika baadhi ya sehemu za dunia zaidi ya miongo miwili iliyopita, wakati asilimia ya vijana ambao walitumia dawa za kulevya kama ni hatari ilishuka kwa asilimia 40.
Pengo la mtazamo bado lipo licha ya ushahidi kwamba matumizi ya bangi yanahusishwa na aina mbalimbali za athari za afya na madhara mengine, hasa kati ya watumiaji wa muda mrefu.
Aidha, nchi nyingi kwa wakati huu zimeelezea kuongezeka kwa matumizi ya bangi wakati wa janga la COVID-19.
“Mtazamo wa hatari ya matumizi ya dawa za kulevya umehusishwa na viwango vya juu vya matumizi ya dawa hizo, na matokeo ya ripoti ya dawa za kulevya ya dunia ya UNODC ya 2021 yanaonesha haja ya kuziba pengo kati ya mtazamo na hali halisi kwa kuelimisha vijana na kulinda afya ya umma,” alieleza mkurugenzi mtendaji wa UNODC, Ghada Waly.
Ripoti hiyo inasema janga la COVID-19 limetumbukiza watu zaidi ya milioni 100 katika umaskini uliokithiri na limesababisha ukosefu wa ajira na kuchochea zaidi pengo la usawa, wakati dunia ikipoteza ajira milioni 114 katika mwaka 2020.
Hali ya matatizo ya afya ya akili hasa miongoni mwa vijana pia inaongezeka duniani kote. Sababu hizi zina uwezo wa kuinua ongezeko la matatizo ya matumizi ya mihadarati.
Aidha, mabadiliko yameshaanza kubainika katika mifumo ya matumizi ya dawa za kulevya wakati wa janga la corona, ikiwa ni pamoja na ongezeko la matumizi ya bangi na matumizi yasiyo ya matibabu ya dawa za usingizi.
Changamoto za kiuchumi pia zinauwezekano wa kuharakisha upanuzi wa soko kwa dawa hizo.
Sambamba na hilo, ripoti hiyo inaonyesha kuwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya wamejikwamua kutoka kwenye athari za mwanzo zilizosababishwa na vizuizi vya kukabiliana na COVID-19.
Wafanyabiashara hao hivi sasa wanafanya kazi tena katika viwango vya kabla ya janga hilo, wakiongozwa na kuongezeka kwa utumiaji wa teknolojia na malipo ya pesa za sarafu.
Upatikanaji wa mihadarati na uuzaji mtandaoni pia umekuwa rahisi zaidi kuliko wakati wowote na masoko makubwa ya dawa kwenye wavuti za kinyemela sasa yana thamani ya dola milioni 315 kila mwaka.
Shughuli za uuzaji wa mihadarati kwa njia isiyo ya ana kwa ana kama vile kupitia barua poepe, pia zinaongezeka, mwenendo ambao huenda umechapuzwa na janga hilo.
Ubunifu wa haraka wa kiteknolojia, pamoja na wepesi na jinsi wasafirishaji na wauzaji wa dawa za kulevya ambao wanatumia njia mpya za mtandaoni kuuza dawa za kulevya na vitu vyengine, kunaweza kuongeza upatikanaji wa dawa haramu.
Kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia wakati wa janga la COVID-19 pia kumesababisha ubunifu katika huduma za kuzuia dawa ya kulevya na matibabu, kwa njia ya mifano rahisi zaidi ya utoaji wa huduma kama vile dawa kwa njia ya simu (telemedicine), kuwezesha wataalamu wa afya kufikia na kutibu wagonjwa wengi zaidi.
Wakati huo huo, idadi ya huduma mpya ya kisaikolojia (NPS) inayojitokeza kwenye soko la kimataifa ilianguka kutoka 213 mwaka 2013 hadi 71 mwaka 2019.
Matokeo haya yanaonyesha mifumo ya udhibiti wa kitaifa na kimataifa imefanikiwa katika kupunguza kuenea kwa NPs katika nchi za kipato cha juu, ambapo mwenendo huo uliibuka kwanza miaka kumi iliyopita.
Ripoti pia imegundua kwamba matumizi ya aina mbili za kitabibu za afya ni dawa zinazotumiwa kutibu watu wenye matatizo ya matumizi ya mihadarati aina ya opioid, methadone na buprenorphine, yamezidi kupatikana, kama matibabu ya msingi ya sayansi kwa kiasi kikubwa.
“Mihadarati inagharimu maisha,” anahitimisha mkuu wa UNODC. “Katika wakati ambao kasi ya habari mara nyingi inaweza kuzidi kasi ya inaweza kuzidi kasi ya kuthibitisha, janga la COVID-19 limetufundisha kwamba ni muhimu kuachana na kelele na kuzingatia ukweli, somo ambalo tunapaswa kuzingatia ili kulinda jamii kutokana na athari za madawa ya kulevya. ”
Kwa upande wake katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema ingawa nchi zinashirikiana kudhibiti usafirishaji haramu wa dawa za kulevya lakini nchi nyingi zenye kipato cha chini zina mifumo dhaifu ambayo inaruhusu biashara hiyo kuendelea. Pia amegusia suala la dawa zinazo dhibitiwa matumizi yake.
Guterres amezihimiza nchi wanachama kutumia takwimu kutafuta suluhu, “uwepo wa takwimu bora utasaidia kutambua mwenendo na kuwezesha ufuatiliaji wa wakati halisi wa njia za usafirishaji zinazohama haraka. Mifumo ya kutoa tahadhari mapema ya kisayansi itasaidia kutabiri vitisho vitakavyo ibuka vya dawa za kulevya”
Uzinduzi wa ripoti ya dawa za kulevya ya dunia ya 2021 umekuja kufuatia hivi karibuni ulimwengu kuadhimisha siku ya kimataifa dhidi ya matumizi mabaya ya dawa za kulevya na usafirishaji haramu.
Kaulimbiu ya mwaka huu wa 2021 ya kampeni inayoongozwa na UNODC ni “Sambaza ukweli juu ya mihadarati, okoa maisha” ili kufikia ulimwengu bila ya matumizi mabaya ya dawa za kulevya.