NA KHAMISUU ABDALLAH

WANAODAIWA kuiibia serikali mabomba 46 ya maji yenye thamani ya shilingi 80,000,000 wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Washitakiwa hao ni Bakar Mohammed Bakar (53) mkaazi wa Jang’ombe, Ali Chande Ali (35) mkaazi wa Kianga na Khalfan Omar Juma (59) mkaazi wa Magogoni wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Wote kwa pamoja walifikishwa katika mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe mbele ya hakimu Fatma Omar na kusomewa shitaka linalowakabili na Mwendesha Mashitaka Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Soud Said.

Ilidaiwa mahakamani hapo washitakiwa hao walipatikana na kosa la kuiibia serikali kinyume na kifungu cha 251 (1) (2) (a) na kifungu 258 na 261 (1) (2) vya sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Mwendesha Mashitaka Wakili Soud alidai kuwa mnamo mwezi Aprili 4 mwaka huu nyakati tofauti huko Saateni wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja washitakiwa hao wote kwa pamoja kwa udanganyifu na bila ya kuwa na dai la haki waliiba mabomba ya chuma 46 yenye thamani ya shilingi 80,000,000 mali ya Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) ambalo ni shirika la umma kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Washitakiwa hao waliposomewa shitaka hilo walilikataa na kuiomba mahakama iwapatie dhamana huku upande wa mashitaka ukidai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Fatma alikubaliana na ombi la upande wa mashitaka na kuiahirisha kesi hiyo hadi Juni 23 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Mahakama pia iliwataka washitakiwa hao kila mmoja kujidhamini mwenyewe kwa shilingi 2,000,000 fedha taslimu na kila mshitakiwa kuwasilisha wadhamini wawili ambao kila mmoja atamdhamini kwa shilingi 500,000 na kuwasilisha vitambulisho vyao vya Mzanzibari Mkaazi na barua ya Sheha wa Shehia wanazoishi zinazoonesha nambari za nyumba.

Mshitakiwa Ali Chande na Khalfan Omar walikamilisha masharti hayo na wapo nje kwa dhamana huku mshitakiwa Bakar alishindwa kujidhamini na kupelekwa rumande hadi tarehe nyengine aliyopangiwa mahakamani hapo.