TIGRAY, ETHIOPIA

WAPIGANAJI kutoka jimbo lililokumbwa na mzozo la Tigray, Ethiopia wameonya kwamba wanajeshi wao watatafuta mbinu za kuharibu uwezo wa vikosi vya Ethiopia na Eritrea, licha ya serikali ya Ethiopia kutangaza sitisho la mapigano la upande mmoja katika jimbo hilo.

Serikali ya Ethiopia ilitangaza sitisho la mapigano kupitia vyombo vya habari vya serekali mwanzoni mwa wiki hii na kueleza kwamba tangazo hilo litaanza kutekelezwa mara moja.

Taarifa ya sitisho hilo la mapigano limejiri baada ya miezi minane ya mzozo huko Tigray, na wakati wanajeshi wa chama tawala cha zamani katika jimbo la Tigray waliingia katika mji mkuu wa jimbo hilo, Mekelle na kulakiwa kwa shangwe na wakazi wa mji huo.

Msemaji wa vikosi vya Tigray ameonya katika mahojiano na shirika la habari la Reuters kwamba wanajeshi wa Tigray wataingia katika nchi jirani ya Eritrea na katika jimbo la Ethiopia la Amhara, kuvisaka vikosi adui iwapo itahitajika.

Baadhi ya waandishi wa habari katika mji wa Mekelle wamesema hawajaona wanajeshi wa serikali ya Ethiopia mjini humo tangu mwishoni mwa wiki iliyopita.