ILI kutoa nafasi ya wadau, washabiki na wapiga kura katika uchaguzi mkuu nwa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), kuwatambua wagombea walioteuliwa kuwania nafasi ya urais wa shirikisho hilo, Zanzibar Leo kwa ridhaa ya wagombea hao inachapisha katika ukurasa huu, maelezo yaliyoandaliwa na wagombea wenyewe.

Katika maelezo hayo, wagombea watapata nafasi kueleza malengo na maoni yao kuhusiana na mchezo wa soka Zanzibar na sababu za kuwania nafasi hizo.

 MGOMBEA: Suleiman Mahmoud Jabir

Kwa nini nagombea Shirikisho la Mpira wa miguu Zanzibar (Zanzibar Football Federation – ZFF) nafasi ya urais?

“Kwa Maslahi ya Mpira na Maendeleo ya Mchezo wa Mpira”

UTANGULIZI

Ni jambo lisilopingika kuwa mchezo wa mpira wa miguu, kandanda, kabumbu au soka ni mchezo maarufu na ndio unaopendwa sana duniani na hata hapa kwetu, Zanzibar.

Mvuto, mwamko, shamra shamra, ushindani, mabishano, furaha na majonzi yanayopatikana katika Mchezo huu, ni mambo ya aina yake ambayo ni nadra sana kuonekana katika Michezo mengine.

Wakati watu walio wengi wanacheza, wanaangalia na kuufuatilia mchezo huu kupitia vyombo vya habari; basi hapana shaka mpira wa miguu, kandanda au soka kwa kiasi kikubwa hugusa nyoyo na hisia za watu wengi wa rika, jinsia, rangi, asili, dini, jamii, tofauti wakiwemo; wachezaji, walimu, wapenzi, mashabiki, viongozi wa michezo, wafanyabiashara, wanasiasa n.k.

Pamoja na hali hiyo, jambo la kusikitisha sana ni kuwa; wakati nchi za wenzetu zinaendeleza Mpira/Soka lao kisayansi sisi Zanzibar tuliendeleza Uongozi dhaifu, kutokuwa na mipango endelevu, kujinufaisha nafsi, usuhuba, migogoro pamoja na mivutano/malumbano na Serikali.

Hasara iliyoje! Tulichovuna ni kuporomoka kwa kiwango cha soka letu, kudharau taaluma za walimu, waamuzi na za kiuongozi, kufukuza wapenzi na mashabiki viwanjani, kuwaondoshea imani na kuwakimbiza wadhamini na matokeo mabaya hususan kwa vilabu vyetu na matokeo ya kushutukiza kwa Timu yetu ya Taifa (Zanzibar Heroes).