NA KHAMISUU ABDALLAH

KAMISHNA Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Salum Yussuf Ali, amewataka wadau wa kodi kujenga ushirikiano na kuondoa dhana ya uadui baina yao.

Kauli hiyo aliitoa wakati akizungumza na Washauri Elekezi wa kodi katika mafunzo yaliyoandaliwa na bodi hiyo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) juu ya mfumo wa utoaji risiti kielektroniki (VFD) yaliyofanyika katika ofisi za bodi hiyo Mazizini.

Alisema washauri wa kodi ni wadau wakubwa kwa mamlaka za ukusanyaji wa mapato ambao wanawategemea katika kuwasaidia jukumu zito walilopewa na serikali yao la ukusanyaji kodi.

Alibainisha kuwa, suala la kodi linahitaji uadilifu mkubwa baina ya wadau hao na watoza kodi ili kuona serikali inapata mapato yake kwa ajili ya kuhudumia maendeleo mbalimbali.

Alisema wanapokuwa waadilifu wao katika majukumu yao basi kwa kiasi kikubwa wanaisaidia ZRB katika kufikia azma ya ukusanyaji wa kodi na kuifikisha katika mfuko mkuu wa serikali.

Kamishna Salum alisisitiza haja ya uzalendo kwa washauri hao na kuainisha changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo ya mapungufu ya watu wanaokusanya kodi na ya kisheria.

Katika hatua nyengine Kamishna huyo aliwapongeza washauri hao kwa kupatiwa vyeti na kuwashauri wale ambao bado hawajajisajili kuhakikisha wanajisajili ili kupatiwa vyeti maalum na kuwa wadau muhimu kwa ZRB na TRA.

Naye Meneja Uhusiano na Huduma kwa Walipa Kodi wa bodi hiyo, Shaaban Yahya Ramadhani, alisema kwa kushirikiana na TRA, wameamua kuwaita washauri elekezi wa kodi ili kuwapa elimu juu ya majukumu yao na nafasi yao hususan katika kipindi hichi ambacho serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato kielektroniki.

Alisema washauri elekezi ndio wenye walipa kodi wengi hivyo ni vyema kutumia nafasi yao hiyo kwa wateja wao katika kuwafahamisha mfumo huo ambao umeshaanza hivyo kuwashajihisha katika kuwaelekeza na kuhakikisha wanafuata sheria ili kuondosha mivutano baina yao na taasisi za kodi.

Ofisa Mwandamizi Elimu na Huduma kwa Walipa kodi wa TRA upande wa Zanzibar, Dk. Shuwekha Salum Khalfan, alisema lengo la mkutano huo ni kutoa elimu kwa washauri wa kodi ambao wanasaidia katika kuhakikisha walipa kodi wanasimamia na kufuata sheria.

Alisema ZRB na TRA wana lengo moja la kukusanya kodi na kupeleka serikalini kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Akizungumzia mfumo wa ukusanyaji kodi kwa njia ya kielektroniki (VFD) alisema, mfumo huo utasaidia kwa kiasi kikubwa walipa kodi kutoa risiti na kuweza kutunza kumbukumbu zao vizuri.

Nao Washauri hao waliipongeza ZRB kuanzisha mfumo huo ambao utasaidia wateja wao kuweza kufuata sheria na kuendana na wakati uliopo kwa kuondokana na changamoto ya kufuata huduma katika bodi hiyo na kuleta urahisi katika ukusanyaji wa kodi.

Katika mkutano huo Kamishna huyo alikabidhi vyeti kwa Washauri Elekezi wa kodi waliosajiliwa kisheria huku mfuko wa utoaji wa risiti za kielektronikI kwa mashine za VFD unatarajiwa kuanza kutumika rasmi Julai 1 mwaka huu.