NA HAFSA GOLO

WATENDAJI wanaosimamia mradi wa kunusuru kaya maskini kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) Zanzibar wametakiwa kufanikisha malengo ya mradi huo ili uwanufaishe wananchi kiuchumi.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Dk. Khalid Salum Mohamed katika kikao maalumu cha kusikiliza changamoto na vikwazo vinavyowakabili walengwa wa mradi huo katika shehia ya Bumbwini Makoba, wilaya ya Kaskazini ‘B’, Unguja.

Alisema ni lazima watendaji hao wahakikishe wanasimamia vyema majukumu waliyokabidhiwa ikiwa ni pamoja na kuwafikia walengwa wote kwani itasaidia kuwakomboa na umasikini.

Alisema, hatua hiyo itasaidia utekelezaji bora na wenye kuondoa malalamiko ya wananchi juu ya serikali yao sambamba na kuona dhamira ya serikali ya kuimarisha maisha ya kaya na kuwaondolea umaskini inafikiwa kwa wakati uliopangwa.

Aidha aliwataka watendaji hao juu kuachana na kufanya kazi kwa mazoea ambao unaleta vikwazo katika utoaji wa huduma bora kwa walengwa na hatimae kuibua matatizo yasiyokuwa na tija wala manufaa kwa serikali.

Hivyo aliwasisitiza watendaji wanaosimamia TASAF kutimiza    masharti na vigezo vilivyowekwa katika kuzifikia kaya hizo huku wakihakikisha wanaachana na tabia za kujifungia ofisini.

Aidha Dk. Khalid, aliahidi kuzisimamia changamoto zinazowakumba wananchi kupitia mradi huo ili wahusika wote wapate stahiki zao kwa mujibu wa taratibu na matakwa ya mradi huo bila ya usumbufu.

Mbali na hilo, Waziri Khalid, alikiri kuwepo kwa changamoto za kiutendaji ndani ya mradi huo sambamba na kuahidi kuunda kamati maalumu ya kufuatilia na kupatiwa ufumbuzi ndani ya kipindi kifupi.

Hata hivyo alitoa agizo kwa watendaji hao kumpatia oradha halisi ya walengwa wote wa Tasaf sambamba na ile ya watu ambao bado hawajahakikiwa ama hawajapatiwa fedha zilizotolewa katika awamu hii.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, Aboud Hassan Mwinyi, alisema atatumia fursa nyengine katika kuwaelimisha masheha juu ya kusimamia haki na wajibu katika majukumu yao ya kazi ikiwemo kufuatilia kwa karibu mradi huo ili walengwa wote wapatiwe fedha kwa mujibu wa taratibu.

Pamoja na hilo, aliwahimiza watendaji hao juu ya umuhimu wa kutimiza majukumu yao ya kazi ipasavyo kwani itasaidia kuondokana na changamoto zisizo za lazima.

Mkurugenzi wa TASAF Zanzibar, Khalid Bakari Amran, alisema moja ya changamoto iliyopo ni pamoja na wananchi kutoitikia wito unaotolewa na masheha.

Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Bumbwini, Mbarouk Juma Khatibu, aliwataka wananchi wanaonufaika na mpango huo kuendelea kujenga matumaini juu ya serikali yao kwani malalamiko na kasoro zote zilizopo ndani ya mradi huo zitafanyiwa kazi.

Aidha alisema atashirikiana na serikali kwa karibu ili kuona changamoto zilizojitokeza kwa walengwa hao zinapatiwa ufumbuzi.

Naye Mwakilishi wa jimbo hilo, Mtumwa Peya alisema anaamini viongozi wa serikali watazifuatilia changamoto zote na muda mfupi zitapatiwa ufumbuzi.

Mapema wananchi walimueleza Waziri kwamba utoaji wa huduma kwa watendaji wa mradi huo ni mbovu jambo ambalo limekuwa likisababisha kuleta usumbufu kwa walengwa.

Walidai moja ya kadhia inayowakumba ni kutohakikiwa ingawa wamefika katika vituo husika na wakati mwengine walengwa waliohakikiwa kutopatiwa fedha zao hadi leo kwa kisingizio cha matatizo ya mtandao.

Aidha katika kikao hicho imeelezwa kaya 915 hazijafanyiwa uhakiki katika utekelezaji wa awamu hii ya mradi huo kutokana na changamoto mbali mbali zilizokuwa nje ya uwezo wao watendaji wa mradi huo.