NA KHAMISUU ABDALLAH, MOHAMMED RASHID, DOMECO
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesema inawachukulia hatua watendaji wote wasiowaaminifu wanaojihusisha na utoaji wa vyeti feki ikiwemo vyeti vya kuzaliwa kwa wananchi wanaotaka huduma hiyo.
Waziri Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Masoud Ali Mohammed alitoa kauli hiyo katika ukumbi wa baraza la Wawakilishi Chukwani, wakati akijibu suala la nyongeza liloulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Wingi, Kombo Mwinyi Shehe, alietaka kujua ni hatua gani zinazochukuliwa kwa watu wanaojihusisha na jambo hilo.
Alisema watendaji ambao sio waaminifu na wengine wakijiita vishoka wamekuwa wakifanya vitendo hivyo kwa kuwadanganya wananchi na kuwachukulia pesa zao.
Aidha alibainisha kuwa wananchi kupatiwa huduma hiyo kunatokana na wao wenyewe kutofika katika Ofisi za usajili wa matukio ya kijamii.
Hivyo, aliahidi kuwa serikali itaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kupata vyeti halali kwa kukifika ofisi husika ili kuondokana kupatiwa vyeti feki.
Nae, Mwakilishi wa Jimbo la Konde, Zawadi Amour Nassor, alietaka kujua sababu gani inayopelekea mtu kutozwa kiwango kikubwa cha fedha pale anapotaka kupatiwa cheti cha shilingi 50000.
Waziri Masoud, alisema cheti cha kuzaliwa hakifikii shilingi 50000 bali wananchi waotozwa fedha hizo ni wale wanakwepa taratibu zilizowekwa kisheria na hawafiki katika ofisi husika.
“Hawa wanaotozwa kiwango hichi cha fedha ndio wale wanaotumia vishoka hivyo ni jambo la msingi wananchi wetu kufuata utaratibu ili waweze kupatiwa vyeti halali,” alishauri.
Hivyo alisema sababu zinazopelekea cheti kuwa si halali inatokana na utoaji wa cheti husika kuwa kimetolewa na wizara au mamlaka husika na kutiwa saini na kiongozi husika ni kutokana na ukiukwaji wa taratibu za kisheria wakati wa upatikanaji wa cheti hicho kwa mujibu wa kifungu namba 26 (1) (2) cha sheria namba 3 ya mwaka 2018 ya Wakala wa Usajili wa matukio ya kijamii.
Alisema sheria hiyo kifungu cha 49 (1) (a) (b) (c) (d) na (e) kimefafanua kukosekana uhalali wa cheti kinachotolewa na wizara au mamlaka husika na kutoa muongozo wa kufuta usajili wa cheti hicho endapo yatajitokeza mambo mbalimbali ikiwemo usajili uliofanywa kutokana na taarifa zisizo sahihi au zilizokamilika.
Mambo mengine alisema ni usajili uliofanyika kwa udanganyifu, uongo au rushwa, cheti cha kuzaliwa, ndoa, talaka, kifo au kitambulisho kinahitajika kuzalishwa tena kutokana na makosa, kujiandikisha mara mbili au zaidi na kuwa amri ya mamlaka ya kufutwa kwa usajili.