NA SAIDA ISSA, DODOMA
MKUU wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweli, amesema Madaktari, Wauguzi na Watumishi wa sekta ya afya wametakiwa kuzingatia haki za binadamu na utawala bora katika utoaji wa huduma.
Shekimweli amesema wakati akifungua Mafunzo ya haki na utawala bora kwa watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo ambapo amesema, Lengo ni kuongeza uelewa kwa watumishi wa sekta ya afya.
Alisema ni vyema watendaji wa sekta ya afya kuifahamu misingi ya utawala bora katika maeneo yao ya kazi ili kutoa huduma bora kwa wagonjwa huku wakiwa na mifumo sahihi ya kufuata na kutoa huduma kwa haraka na kuwaondolea usumbufu wananchi
“Na kwa kutambua mchango huu muhimu wa sekta ya afya katika ustawi na maendeleo ya nchi Serikali inaendelea kuboresha na kuimarisha hali ya huduma za afya nchini kwa kuongeza miundombinu, vifaa, watoa huduma ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya utendaji kazi na msalahi yao,”alisema
Aidha alisema uwajibikaji wenye kuzingatia utaalam, sheria, kanuni, na miongozo ndio msingi kwa sekta ya afya katika kutoa huduma bora inayokidhi mahitaji.
Alieleza kuwa Katika utekelezaji wa haki za binadamu Serikali ina wajibu wa kutimiza haki kwa kuweka miundombinu, sheria, kanuni, sera pamoja na mipango ya muda mfupi na mrefu kwa nia ya kuhakikisha na kuwezesha utekelezaji na upatikanaji wa haki ya afya nchini.
Naye Kamishna wa Tume ya hiyo Dk. Fatma Khalfan akizungumaza Katika Mafunzo hayo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu, alisema mafunzo hayo inafungua mlango wa mashirikiano kati ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na Tume.
“Lengo hasa la kuandaa na kuwasilisha mafunzo haya kwa watumishi wa sekta ya afya ni kuwawezesha kuitambua, kuielewa, kuijua na kuiishi Misingi ya Utawala Bora na pia haki za Binadamu na chimbuko lake na kutumia mafunzo haya katika kuleta ufanisi na tija katika utoaji wa huduma ya afya,”alisema.